Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilio cha wafanyabiashara kodi chasikika

Samia Mszz Kilio cha wafanyabiashara kodi chasikika

Tue, 30 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imesikia kilio cha wafanyabiashara na kuahidi kuwa itaunda kamati ya kupitia mifumo ya kodi kwa ajili ya kushughulikia tatizo hilo ili kuweka mazingira mazuri ya kundi hilo katika ufanyaji kazi wao.

Rais Samia Suluhu Hassan alisema hayo jana Ikulu, Dar es Salaam, katika mkutano wa 15 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) baada ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), kueleza changamoto wanazokutana nazo wafanyabiashara zikiwamo kufungiwa akaunti za benki, kuchukuliwa fedha bila utaratibu sahihi na kufungiwa mashine za kutoa risiti (EFD).

Mkutano huo uliongozwa na Rais Samia na kuhudhuriwa na wajumbe wa baraza hilo na wawakilishi kutoka vyama vya wafanyabiashara, wawekezaji na watendaji wakuu wa kampuni binafsi.

Akifungua mkutano huo, Rais Samia alisema hivi karibuni alifanya kikao na baadhi ya wafanyabiashara kusikiliza kero zao na suala la kodi lilijitokeza.

Kutokana na hali hiyo, alisema serikali imeamua kuunda kamati itakayopitia mfumo mzima wa ulipaji kodi, ikiwamo utekelezaji wa sera na sheria ili kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na hatimaye wanufaike na kufurahia shughuli wanazofanya.

“Serikali imedhamiria kuondoa hizo changamoto kwa hiyo tutaunda kamati itakayoshirikisha wajumbe kutoka serikalini na sekta binafsi, mpitie kwa undani halafu mtuletee mapendekezo na ushauri mtakaoona unafaa,” alibainisha.

Rais alisema anafahamu bado kuna changamoto katika maeneo mbalimbali ikiwamo baadhi ya watendaji wa serikali kutoelewa dhamira ya kuwezesha biashara na uwekezaji, stempu za kodi na uchelewashaji wa vibali.

Pia alimwagiza Waziri wa Viwanda na Biashara na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufanya kazi kwa karibu na wafanyabiashara na wawekezaji, ili kutatua changamoto zinazowakabili na wameshaanza kazi hiyo.

Alisema kupitia falsafa ya R4, serikali inaendelea kuboresha mazingira ya biashara na kukuza uwekezaji hususan vijijini ambako ndiko kunahitaji nguvu zaidi kwa sasa na kutoa kipaumbele kukuza biashara ya kikanda na kimataifa.

“Hivyo basi nawataka wakuu wa mikoa na wilaya wa mipakani kuhakikisha biashara mipakani zinafanyika kwa wepesi kwa kuondoa vikwazo na vizuizi visivyo na lazima,” aliagiza.

Alisema tangu kuanzishwa kwake, TNBC imekuwa muhimu kwa kuishauri serikali namna bora ya kuboresha mazingira ya biashara, ikiwamo kuboresha sera, sheria na taratibu za biashara na uwekezaji.

Rais alisisitiza Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kuiunganisha mifumo hiyo na kuhakikisha kuwa ifikapo Desemba 2024 mifumo yote mipya na ya zamani inasomana ili kurahisisha utoaji huduma kwa sekta binafsi na wadau wengine.

Alisema pamoja na changamoto za kidunia, uchumi wa nchi bado ni himilivu, kukua na kuimarika zaidi. Alisema mwaka 2023 ulikua kwa asilimia 5.2 ikilinganishwa na asilimia 4.7 ya mwaka 2022 huku mfumuko wa bei ukiwa asilimia tatu ikiwa ni ndani ya malengo na utoshelezi chakula ni zaidi ya asilimia 120.

Hali hiyo, alisema imewezesha kukuza biashara na kuvutia uwekezaji zaidi, kwa kuwa tangu Julai, 2021 hadi Juni, 2024 miradi mikubwa 1,350 ya uwekezaji yenye thamani ya Dola za Kimarekani bilioni 14.2 ilisajiliwa na kutarajiwa kuzalisha ajira 324,381.

Alisema kupitia falsafa ya R4, serikali imekuja na mageuzi ya kuondoa ukiritimba katika uendeshaji wa shughuli za reli kwa kurekebisha Sheria ya Reli, ili kuruhusu waendeshaji binafsi kutumia miundombinu hiyo kutoa huduma za usafirishaji.

Mwakilishi wa Mwenyekiti wa TPSF, Ally Amour, alisema changamoto hizo za kikodi zinatokana na udhaifu katika usimamizi wa sheria ya kodi, jambo linaloharibu uhusiano kati ya wafanyabiashara na TRA.

Alisema katika kikao na wafanyabiashara hao waligundua kuwa kuna wafanyabiashara waliokuwa na madeni ya kodi na waliingia makubaliano ya kulipa na wakakiuka, hivyo kwa mujibu wa sheria TRA ilikuwa sahihi kuwaandikia barua ya kuwakumbusha kulipa deni haraka.

Pia walibaini kuna wafanyabiashara waliokuwa na madeni makubwa ya nyuma na hawakuwa na makubaliano na TRA ya namna ya kulipa hivyo hali iliyosababisha kuandikwa barua hizo.

Amour alisema kuna wafanyabiashara ambao hawakuwa na deni lolote na hivyo hakukuwa na haja ya kuwaandikia barua ya kukumbusha kulipa madeni. Pia alisema waliona kuna upungufu katika kufanya tathmini ya mizigo bandarini na kamata zilizokuwa zinaendelea Kariakoo zilikuwa zinashinikiza utolewaji wa risiti za EFD.

Pia alisema walibaini kuna ongezeko la biashara za magendo hasa za bandia ambalo linaathiri ushindani wa biashara nchini, na walishakutana na kamishna wa TRA kujadili namna ya kukabiliana na suala hilo na kuongezwa wigo wa ulipaji kodi.

Aidha, alisema ofisi ya msuluhishi wa malalamiko ya taasisi ya kikodi kuwa chini ya TRA itasababisha isitekeleze majukumu yake kwa weledi na kushauri iwe huru ili kupunguza malalamiko ya wafanyabiashara.

Pia alishauri kutafuta suluhu ya sekta isiyo rasmi ili iwe rasmi kwa ajili ya kuongeza wigo wa walipa kodi kufikia asilimia 10 ya Watanzania.

Alisema uhaba wa dola ya kimarekani bado unaathiri biashara nchini kwa sababu wanashindwa kununua malighafi za viwandani, upatikanaji wa mafuta na kushauri serikali ipunguze matumizi ya fedha hiyo katika kununua bidhaa zinazozalishwa nchini.

Alishauri pia wafanyabiashara wasigeuzwe kuwa maadui, kutengenezewa mizengwe na figisu pale wanapotoa ripoti ya masuala ya rushwa na upotevu wa mapato kama ilivyotokea Arusha kwa mfanyabiashara ambaye ni mwanachama wao.

Aidha, alisema sekta binafsi itaendelea kufanya kazi kwa weledi na kuchangamkia fursa ndani na nje ya nchi na kulipa kodi.

Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi, alisema kupitia mkutano huo imedhihirika kuwa wafanyabiashara wako tayari kulipa kodi kwa mujibu wa sheria kwa kufahamu kuwa hakuna nchi inayoweza kupata maendeleo bila kukusanya kodi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, alisema ofisi hiyo kwa kushirikiana na TNBC imeratibu na kuwezesha mikutano yote ya mabaraza ya biashara iliyofanyika katika mikoa mbalimbali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live