Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilimo wapongezwa kwa kufuta vyama vya ushirika 2,539

04253e8be2415be3b30afb3a91977b38.png Kilimo wapongezwa kwa kufuta vyama vya ushirika 2,539

Tue, 4 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WIZARA ya Kilimo imepongezwa kwa uamuzi wa kuvifuta vyama vya ushirika 2,539 ambavyo vilikuwa na utendaji mbovu uliosababisha kero kwa wanaushirika nchini na kukwamisha tija.

Pongezi hizo zimetolewa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu ( Uwekezaji), Angellah Kairuki wakati alipohutubia wananchi wa Simiyu kwenye Maonesho ya Nanenane ikiwa ni siku maalumu ya kuhamasisha ushirika.

Alisema hatua hiyo ya wizara itawezesha wanaushirika ambapo ni wakulima, wavuvi na wafu gaji kunufaika na kazi zao ndani ya ushirika na wale waliokuwa wakisuasua kujua nini kitawakuta wakiendelea kuwa na utendaji mbovu .

"Ninawapongeza sana Wizara kwa hatua mliyochukua ya kuvifuta vyama vya ushirika 2,539 kwa sababu ya kutofanya kazi iliyokusudiwa.” alisema Waziri Kairuki.

Alisema kukiwepo na vyama vya ushirika vyenye nguvu hata uanzishaji wa viwanda unakuwa rahisi. Akifafanua zaidi Waziri Kairuki alisema katika kipindi cha 2018/2019 jumla ya viwanda 75 vimeanzishwa na vyama vya ushirika vinavyochakata alizeti, chikichi, kutengeneza samani za majumbani, kuchakata pamba na mazao ya nafaka pamoja na usindikaji wa maziwa.

“ Viwanda vinavyomilikiwa na vyama vya ushirika vimeongezeka kutoka viwanda 133 mwaka 2018 hadi kufikia viwanda 208 mwaka 2019” alisema Waziri Kairuki.

Katika hatua nyingine Waziri Kairuki ameiagiza Tume ya Maendeleo ya Ushirika kushirikiana na Wakala wa Serikali Mtandao (EGA) kuangalia namna bora ya kuweka mfumo shirikishi wa TEHAMA utakaoweza kuongeza uwazi katika usimamizi wa vyama vya ushirika hususan AMCOS.

Naye Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alisema wizara yake itaendelea kuhakikisha wakulima, wavuvi na wafugaji nchini wanajiunga na vyama vya ushirika ambavyo vitawasaidia kupata nguvu ya kuweza kupata mitaji,masoko,pembejeo na huduma za ugani ili wakuze uzalishaji.

Maonesho ya Kilimo ya Nanenane Kitaifa yameingia siku ya tatu jana ambapo wananchi na wakulima toka mikoa ya Mara,Simiyu na Shinyanga wanaendelea kupata elimu kwenye mabanda na vipando vilivyoandaliwa.

Kauli mbiu ya Nanenane mwaka huu inasema “ Kwa Maendeleo ya Kilimo,Mifugo na Uvuvi Chagua Viongozi Bora 2020.”

Chanzo: habarileo.co.tz