Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilimo kukutana na wafanyabiashara ya nafaka kujadili fursa za masoko

C09bfd1594717fb0caf52f5782074e30 Kilimo kukutana na wafanyabiashara ya nafaka kujadili fursa za masoko

Sat, 13 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda leo anakutana na wafanyabiashara wa mazao ya nafaka kujadili fursa za masoko.

Hatua hiyo inafanyika wakati Serikali inazidi kuimarisha matumizi ya pembejeo katika kilimo na hivyo kuwepo na uzalishaji wa ziada.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo matumizi ya mbegu bora nchini yalitoka tani 36,614 mwaka 2015 hadi tani 71,208 mwaka 2020 na mbolea kutoka tani 302,450 hadi tani 586,604

Imeelezwa kuwa serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika Kilimo, kati ya mwaka 2015 na 2020, wa kiasi cha takribani Sh bilioni 66 kwa ajili ya kutoa elimu ya kilimo cha kisasa na Sh bilioni 53.2 katika kupeleka mbegu kwa wakulima na sasa kuna matokeo chanya ya kuongezeka kwa tija na kusababisha uwapo wa ziada katika nafaka.

Pamoja na ziada hiyo, serikali pia imetumia takribani Sh bilioni 37.2 kuhamasisha upatikanaji wa masoko ya mazao ya kilimo wakati kumekuwepo na ongezeko la matrekta kutoka 18,460 hadi 25,032 na hivyo kuwepo na kilimo cha kisasa zaidi.

Kutokana na kuendelea kuimarika kwa uzalishaji katika kilimo cha kawaida na kwenye kilimo cha umwagiliaji na kuongezeka kwa tija mfano mpunga kutoka tani 1.8 - 2.0 hadi 4 - 5 kwa hekta serikali inaendelea kutafuta suluhu ya soko la wakulima katika mazao anuai hasa nafaka ambazo zimefurika.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya kilimo, mkutano huo umeitishwa kwa lengo la kuhakikisha kwamba mabadiliko makubwa yanayotokea katika kilimo nchini yanaendelea kuimarishwa kuwapo kwa masoko yenye uhakika.

Mapinduzi ya kijani ya India yalihusisha matumizi makubwa ya pembejeo za kilimo hali iliyosababisha kuongezeka kwa uzalishaji mkubwa wa mazao na serikali ikawa na kazi ya ziada ya kuwezesha soko la mazao ya wakulima.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Kilimo mkutano huo utafanyika katika ukumbi wa hoteli ya Morena jijini Dodoma kuanzia saa tatu asubuhi.

Ilielezwa kuwa Waziri wa Kilimo anawaalika wafanyabiashara wa mazao ya nafaka kwenye mkutano huo ili kwa pamoja kujadili fursa za masoko ya mazao ya nafaka. Aidha Mkutano huo unaitishwa wakati serikali ina mpango wa kuimarisha masoko ya mazao (mahindi) na kuhamasisha uwekezaji wa ujenzi wa viwanda vikiwemo vya mbolea ndani ya nchi.

Chanzo: habarileo.co.tz