Verified Waziri wa Kilimo Hussein Bashe leo ametoa hotuba kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara hiyo kwa mwaka 2023/2024 Bungeni Dodoma ambapo amesema Sekta ya Kilimo kwa mwaka 2021 ilikua kwa asilimia 3.9 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.9 mwaka 2020, vilevile Sekta ya Kilimo imechangia asilimia 26.1 katika Pato la Taifa, imetoa ajira kwa Wananchi kwa wastani wa asilimia 65.6 na kuchangia asilimia 65 ya malighafi za viwanda.
Bashe amesema “Sekta ya Kilimo kwa upande wa mazao ilikua kwa asilimia 3.6 mwaka 2021 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 5 mwaka 2020; imechangia asilimia 14.6 kwenye Pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 15.4 mwaka 2020; na imeendelea kuchangia asilimia 100 ya upatikanaji wa chakula”
“Aidha, mazao ya kilimo yamechangia takriban Dola za Marekani Bilioni 1.38 ya mauzo nje ya nchi. Ukuaji na mchango wa Sekta ya Mazao kwa mwaka 2021, umeshuka kutokana na athari za UVIKO – 19 na vita kati ya Urusi na Ukraine ambazo ziliathiri uzalishaji, upatikanaji wa pembejeo za kilimo na masoko ya mazao ya kilimo, pia katika kipindi hicho mabadiliko ya tabianchi yameathiri uzalishaji wa mazao ya kilimo”