Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilimo chanyooshewa kidole kuharibu misitu

41541 Pic+mkaa Kilimo chanyooshewa kidole kuharibu misitu

Thu, 14 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati wadau wakichambua madhara ya mkaa kwa mazingira, imedaiwa kwamba shughuli za kilimo nazo zinachangia kwa kiasi kikubwa katika uharibifu wa mazingira na hasa ukataji wa miti.

Kilimo kimeajiri karibu asilimia 70 ya Watanzania wengi wanaoishi vijijini, huku kikichangia asilimia 29 ya Pato la Taifa, lakini kutokana na mbinu na zana hafifu na uwekezaji wa Serikali katika sekta hiyo kuwa mdogo, tija yake haijaonekana vya kutosha.

Kumekuwa na kaulimbiu mbalimbali za kuhamasisha kilimo ambazo ni pamoja na Siasa ni kilimo, Kilimo Kwanza na sasa kuna Mpango wa Maendeleo ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDPII), yote ikilenga kukuza kilimo.

Lakini mikakati hiyo inaangaliwa kwa tahadhari na baadhi ya wadau wa misitu.

Akizungumza katika Jukwaa la Fikra lililoandaliwa na kampuni ya Mwananchi Communications Ltd lililofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, mkurugenzi mkuu wa shirika la kuhifadhi misitu ya asili (TFCG), Charles Meshack alisema kilimo ndicho kinachoongoza kwa kuharibu misitu kwa asilimia 80.

Wakati Meshack akisema hayo, wadau wa mazingira wanauona mkaa kama tishio kubwa zaidi kwa ustawi wa misitu.

Taarifa za hivi karibuni zinaonyesha kuwa Tanzania imefunikwa na misitu kwa asilimia 39. Hata hivyo, kumekuwa na uharibifu wa misitu kwa asilimia moja sawa na hekta 400,000 kwa mwaka ikiwa ni mara mbili ya kiwango cha dunia ambacho ni asilimia 0.5 kwa mwaka.

Miongoni mwa sababu kubwa za uharibifu wa misitu ni mahitaji ya nishati. Taarifa za nishati nchini kwa mwaka 2010 hadi 2012 zinaonyesha kwamba, mwaka 2011 ilikadiriwa kuwa asilimia 90.8 miti iliyovunwa Tanzania ilitumika kwa nishati, huku ikielezwa kuwa kiasi kikubwa cha miti hiyo huchomwa mkaa.

Lakini akizungumzia uharibifu wa misitu, Meshack alisema sababu kubwa ya ukatwaji wa miti ni uanzishwaji wa mashamba mapya, “tusijidanganye kuwa mkaa unaharibu misitu. Kilimo kinaharibu misitu kwa asilimia 80, misitu ni asilimia 13 tu,” alisema Meshack na kushauri kurasimishwa kwa sekta ya mkaa akitaka iwe na chombo maalumu cha udhibiti.

“Lazima turasimishe mkaa, misitu, kama ilivyo Ewura (Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji) kiwe na taasisi huru itakayodhibiti mkaa,” alisema.

TFCG yenye mradi wa mkaa endelevu katika wilaya za Kilosa na Mvomero Mkoa wa Morogoro imewezesha baadhi ya wanavijiji kunufaika kwa kupanda misitu kwa ajili ya mkaa peke yake.

Meshack ameitaka Serikali kuunda sera ya kudhibiti matumizi ya mkaa kwa kuwa ni sekta kubwa inayoajiri watu wengi na kutoa mchango mkubwa katika uchumi.

“Mkaa ni sekta kubwa lakini hauna sera, hilo linapaswa kuangaliwa na Serikali. Kuzuia mkaa siyo suluhisho, ukizuia ndio umemaliza misitu, kwani kitakachofuata ni kufungua mashamba,” alisema Meshack.

“Kuna hekta zaidi ya milioni 20 za misitu zilizohifadhiwa vijijini. Ukizuia kuchoma mkaa bado utakuwa hujamaliza tatizo kwani kitakachofuata ni kufungua mashamba.”

Alisema hata matumizi ya gesi pia si suluhisho la kudumu la kulinda misitu, bali watu wapewe motisha ili wasikate miti.

“Kule vijijini kuna watu wana mashamba pori. Shamba likichukuliwa miti haifidiwi, ila inayofidiwa ni ‘pine’ na mitiki,” alisema.

Alisema kutokana na ongezeko kubwa la watu, kila siku miti 14,900 hutoweka na kwa kasi hiyo misitu itakwisha ifikapo mwaka 2060, kama hakutakuwa na juhudi za kudhibiti.

“Tunakata miti ya asili halafu tunapanda miti mipya, kupanda miti mipya sio suluhisho kwani miti ya asili inajiotea yenyewe. Ni bora tuwe na misitu ya kuvuna mkaa,” anasema.

Katika maoni yake, mtafiti wa mazao ya misitu, Edward Maduhu aliesema njia pekee ya kuzuia biashara ya mkaa wa miti ni kuiingiza kwenye mfumo wa kodi.

Awali, washiriki wa jukwaa hilo walieleza kuwa mkaa ni janga la Taifa na kushauri njia mbalimbali za kudhibiti nishati hiyo.

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Marwa Samuel alishauri kuwa mkaa unapaswa kutangazwa kama janga la kitaifa kutokana na kusababisha uharibifu wa mazingira.

Ili kuokoa jahazi, mshiriki mwingine, Eramson Mambo alishauri kuwepo na mkakati wa matumizi ya mkaa wa miti ya mianzi kwa sababu inakomaa kwa muda mfupi na shina lake linadumu kwa zaidi ya miaka 60.

Lakini mtafiti wa nishati mbadala, Edward Maduhu alishauri uwepo mkakati wa kuweka kodi katika uuzwaji wa mkaa ili kudhibiti nishati hiyo na kuongeza pato la Serikali.

Alisema kama mkaa utalipiwa kodi kwa usawa, matumizi yake yatapungua na mkaa mbadala utaingia sokoni na kuokoa mazingira.

“Tuwekeze kwenye ujenzi wa viwanda vya mkaa mbadala, inawezekana,” alisema Maduhu.

Alisema matumizi hayo yatasaidia kuzuia uvunaji holela wa miti kwa sababu ya mkaa.



Chanzo: mwananchi.co.tz