Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilimo ‘chaibeba’ Tanzania uchumi wa kati

Kilimo Kilimo ‘chaibeba’ Tanzania uchumi wa kati

Mon, 13 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

TAASISI ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI), Kituo cha Uyole jijini Mbeya, kimesema sekta ya kilimo imechangia kwa kiwango kikubwa kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kati unaochagizwa na maendeleo ya viwanda.

Hayo yalisemwa juzi na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo hicho, Dk. Tulole Bucheyeki, alipokuwa anakagua maandalizi ya vipando vya mazao mbalimbali kwa ajili ya Maonyesho ya Wakulima (Nanenane) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yanayotarajiwa kufanyika katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Alisema viwanda vingi ambavyo vimeanzisha hapa nchini vinategemea malighafi zinazotokana na mazao mbalimbali ambayo mengi yanazalishwa ndani ya nchi na hivyo akasisitiza kuwa taasisi hiyo itaendelea kutoa mafunzo kwa wananchi ili waimarishe zaidi uzalishaji.

Alisema kwa sasa taasisi hiyo imegundua teknolojia zaidi ya 40 ambazo zitasaidia wakulima kuongeza uzalishaji wa mazao ambao utaliwezesha taifa kujitosheleza kwa chakula, malighafi za viwandani na ziada kuuzwa nje ya nchi.

“Kutokana na umuhimu wa kilimo, tumeamua kuwasaidia wananchi kujifunza teknolojia mbalimbali za kilimo kwa mwaka mzima kuanzia Agosti mosi mwaka huu, miaka iliyopita wananchi walikuwa wanaishia kujifunza kwenye maonyesho ya Nanenane pekee,” alisema Dk. Bucheyeki.

Alisema mbali na teknolojia walizobuni pia wamezalisha mbegu za mazao mbalimbali ambazo zitasambazwa kwa wananchi na kuelekezwa mbinu za kisasa za uzalishaji.

Dk. Bucheyeki alisema taasisi hiyo inawakaribisha wananchi wa maeneo mbalimbali kwenda kujifunza teknolojia za kilimo kwenye taasisi hiyo wakati wowote hata kama sio msimu wa kilimo.

Pia alisema taasisi hiyo ina maabara ya kisasa ya kupima virutubisho mbalimbali vilivyomo kwenye udongo ili kuwashauri wananchi kulima mazao kulingana na aina ya udongo wa kwenye mashamba yao.

Baadhi ya wananchi waliotembelea mashamba ya taasisi hiyo kwa ajili ya kujifunza, walisema mafunzo wanayoyapata yamewasaidia kuondokana na kilimo cha mazoea ambacho kilikuwa ni kwa ajili ya kujikimu kwa chakula na sasa wanazalisha kibiashara.

Zawadi Mzumbwe kutoka Kata ya Isuto Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, alisema awali kabla hawajaenda kujifunza kwenye taasisi hiyo, walikuwa wanatumia mbegu za asili ambazo tija yake ilikuwa ndogo.

Alisema walikuwa wanapata kuanzia gunia tatu mpaka saba za mahindi kwenye ekari moja lakini baada ya kupata mafunzo ya matumizi ya mbegu za kisasa na mbinu za kilimo bora wanapata kuanzia gunia 15 na kuendelea.

“Tulikuja kama kikundi tukajifunza kilimo cha kisasa, walituuzia mbegu bora ambazo baada ya kuanza kuzitumia tulibaini kuwa zina tija kubwa maana wao wanasema unaweza ukavuna mpaka gunia 35, sasa hivi tumekuja kujifunza kilimo cha viazi mviringo,” alisema Mzumbwe.

Mzumbwe aliwashauri wananchi wa maeneo mengine ya mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kwenda kupata mafunzo kwenye taasisi hiyo ili kuboresha kilimo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live