Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilimo cha umwagiliaji kinavyowabadili wakulima wa alizeti

Kichwa Cha Alizeti Kabla Ya Kukomaa Kilimo cha umwagiliaji kinavyowabadili wakulima wa alizeti

Tue, 12 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakulima zao la alizeti katika Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, wameeleza namna kilimo cha kisasa kinachohusisha umwagiliaji kinavyowanufaisha, katika kipindi ambacho dunia inashuhudia mabadiliko ya tabianchi.

Kilimo hicho kinahusisha umwagiliaji, upimaji udongo maabara, upandaji unaozingatia nafasi, sambamba na matumizi ya mbolea na mbegu bora za kisasa.

Wakizungumza na waandishi wa habari waliowatembelea mwishoni mwa wiki kwenye mashamba yao yaliyopo kijiji cha Mkoka wilayani humo, wamesema aina hiyo ya kilimo imewasaidia kubadilisha mnyororo mzima wa uzalishaji ukilinganisha na hapo awali.

"Kabla ya kuingia kwenye kilimo hiki, mavuno yalikuwa hayaridhishi. Tulikuwa tunapata gunia tatu hadi tano za alizeti kwa kuwa tulikuwa hatujui hata ukubwa wa shamba na tulikuwa tunalima kwa mazoea," amesema Oznieli Abednego, Katibu wa kikundi cha Umoja wa Umwagiliaji Mkoka chenye wanachama 25.

Abednego amesema tangu wamejitosa kwenye kilimo hicho Agosti mwaka huu, wamefanikiwa kuvuna gunia 75 za alizeti, jambo ambalo ni faida kwao kwa kuwa hawakuwa wanapata idadi hiyo kabla.

Amesema walilima kwenye shamba la ekari 25 na kuanzia sasa watalima mara mbili kwa mwaka, moja kupitia mvua za msimu na nyingine umwagiliaji kupitia mto Mkoka.

"Elimu ya kilimo bora tuliyoipata kutoka Shirika la Kilimo la nchini Denmark (Adda) linalofanya kazi na Taasisi ya Kuboresha Mifumo ya Kilimo nchini (AMDT), imetuwezesha kugeukia kilimo hiki chenye faida lukuki," amesema.

Akielezea mafanikio amesema kama kikundi wamenunua trekta, guta na maisha yao yamebadilika. Amesema hata mwitikio umeanza kuwa mkubwa kutoka kwa wakulima wengine kutaka kuhamia kwenye aina hiyo ya kilimo.

"Niwashauri wakulima wenzangu popote pale walipo mabadiliko ya tabianchi yapo na tukitegemea mvua za misimu tutashindwa. Tunaweza kulima kilimo cha umwagiliaji na tukapata faida kwa kuwa kuna uhakika," ameshauri Abednego.

Kauli yake inaungwa mkono na mkulima, Victoria Mwelya aliyesema fursa ya mto uliopo kijiji hapo, mafunzo pamoja na matenki waliyowekewa na wafadhili, yamewawezesha wao kulima alizeti kwa faida.

"Sasa hivi naweza kulima kitalaamu naweza kupanda kwa nafasi, namwagilia, ni hatua kubwa ukilinganisha na awali nilipokuwa nalima kwa kuchanganya mbegu. Najivunia naweza kuwa mwalimu kwa wanawake wenzangu. Kingine najivunia mafanikio yanagusa hadi familia yangu", amebainisha Mwelya.

Wakati Mwelya akiyaeleza hayo, kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Mkoka (Mviwata), Omary Mpapati, amesema kwa elimu waliyoipata kutoka shirika hilo itawawezesha kuendelea kuwanufaisha kama wakulima.

"Mwanzo tulikuwa tunalima kiholela tulikuwa tunapata gunia moja hadi debe tatu kwa ekari moja kwa kuwa tulikuwa tunachanganya alizeti na mazao mengine kama mahindi na bila ya utaalamu wowote, ila kwa sasa tumebadilika," amesema Mpapati.

Naye, Frank Chipanta kutoka ADDA amesema mradi walioutekeleza, umewaimarisha wakulima kuanzia uzalishaji wa mbegu, uwezeshaji vikundi, mafunzo na mitandao ya wakulima.

Mkakati wa AMDT

Awali akizungumza na waandishi hao kwenye warsha iliyofanyika jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa AMDT Charles Ogutu, alisema wanachotaka ni kuchangia hadi ifikapo mwaka 2030 sekta ya kilimo nchini ikuwe kwa asilimia 10 kutoka 4 iliyopo sasa kama ilivyo ndoto ya Wizara.

"AMDT dhamira yetu ni kuchangia katika Taifa ndio maana tumejikita kwenye mazao ya kimkakati yenye umuhimu zaidi ya alizeti, mahindi na jamii ya mikunde. Ndio maana tumegeukia kilimo cha kisasa kikijumuisha umwagiliaji yaani kuzalisha nje ya msimu," amesema.

Ogutu amesema dhamira ni mkulima azalishe mwaka mzima tena mazao mengi katika eneo dogo akitolea mfano wanavyofanya nchi za Ukraine na Urusi.

"Sekta hii ndio sekta mama imechangia ajira isiyopungua asilimia 65, hivyo tunataka iwe sekta endelevu kwa kubadilisha mfumo mzima wa soko lake ili wakulima wanufaike," amebainisha Ogutu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live