KILIMO biashara katika ushirika ni nyenzo muhimu ya kubaini na kutumia fursa za kibiashara kuwekeza kwenye kilimo ili kupata tija; ni mfumo ambao mkulima hujishughulisha na kilimo kama ofi si-mtaji kikiwa ajira rasmi.
Kilimo hiki cha kisasa huzingatia utaalamu kwa kutumia mbegu bora, mbolea, dawa huku kikizingatia mnyororo wa thamani na kuepusha upoteaji wa mazao shambani, katika usafirishaji au hata kuepusha mazao kuharibika yanapohifadhiwa.
Hujikita pia katika upatikanaji wa soko la uhakika. Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya anasema ushirika ni moyo wa uchumi wa mwananchi mmoja mmoja katika ngazi ya kijiji, kata, tarafa, wilaya, mkoa hadi taifa hivyo, serikali ipo pamoja na wanaushirika kuhakikisha ushirika unaimarika kwa manufaa ya kiuchumi kwa wanaushirika na pia kwa pato la taifa kupitia kodi.
“Serikali inapata kodi kutoka vyama vya ushirika kupitia mauzo ya mazao ndani au nje ya nchi,” anasema. Anatoa mfano wa korosho pekee akisema katika msimu wa Mwaka 2019/2020, serikali ilikusanya ushuru wa zaidi ya Sh bilioni 12.7.
“Ushirika ni moyo wa uchumi wa nchi; ukitazama katika mazao tuliyo nayo zaidi ya 95… Mapato yatokanayo na mazao haya yanasaidia serikali kupiga hatua za nyingi na kubwa kiuchumi,” anasema Kusaya na kuongeza kuwa, ushirika imara na uendelezaji kilimo cha biashara husaidia kuongeza ajira kwa jamii.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji anasema kutokana na manufaa ya ushirika ukiwemo wa kilimo cha biashara, ni wajibu wa wanaushirika kufuata kanuni na mbinu bora za utunzaji wa mazingira ukiwamo upandaji miti, kilimo mseto, kilimo cha umwagiliaji na jitihada nyingine za uhifadhi wa mazingira ili kilimo nchini kiwe chenye tija zaidi na endelevu kwa kutoa chakula cha kutosha na ziada kuuzwa nje.
“Ili tufanikiwe, lazima tuwe na mbinu bora za utunzaji wa mazingira maana wote tunaathirika mazingira yanapokuwa siyo rafiki,” anasma.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC), Theresia Chitumbi anaipongeza serikali kwa kuchukua hatua kali dhidi ya viongozi wa vyama vya ushirika wanaotumia vibaya fedha na mali za wana ushirika. Anatoa pongezi hizo wakati wa kuhitimisha sherehe za Maadhimisho ya 19 ya Ushirika yaliyokuwa na kaulimbiu: “Ushirika kwa mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.”
Chitumbi anasema shirikisho hilo limeanzisha mpango mkakati wa kuhamasisha wanaushirika na kuratibu uanzishwaji wa benki ya ushirika nchini.
“Kuanzishwa kwa benki hii kutasaidia wanaushirika kuongeza mitaji katika uzalishaji wa mazao mbalimbali,” anasema na kuongeza kuwa, benki hiyo itasaidia kuendeleza vikundi vya wanaushirika vya kilimo cha biashara ambacho kimeonesha mafanikio makubwa kimasoko na kutoa bei nzuri kwa mazao.
Kwa msingi huo, anaomba serikali iendelee kurejesha mali za ushirika zilizotaifishwa na kwani zitasaidia kuimarisha juhudi za wanaushirika nchini. Naye Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Dk Benson Ndiege, anasema ili kupata mafanikio katika sekta ya ushirika nchini, watendaji wake wanapaswa kufanya kazi kwa kasi na weledi wa hali ya juu.
Dk Ndege anasema: “Ni muhimu kwa mwanachama mmoja mmoja kupata manufaa katika chama chake cha ushirika na ni wakati kwa vyama vya ushirika kuwajibika zaidi kwa wanaushirika.”
Mshauri wa biashara wa shirika lisilo la kiserikali la kimataifa linaloshughulikia sekta ya ushirika katika nchi mbalimbali duniani la Agriterra, Raymond Lyimo anasema moja ya miradi yake ni kusaidia vyama vya ushirika kuhusu mabadiliko ya tabianchi na kwa sasa upo Tanzania, Uganda na Kenya.
Lyimo anasema mradi huo umeanzishwa mwaka 2019 ili kutoa ruzuku kwa vyama vya ushirika vinavyozalisha mazao yanayostahimili ukame kwa kilimo cha biashara yakiwamo maharage, viazi mviringo, mtama na alizeti.
“Mradi unatoa ruzuku ambayo kwa kiwango cha juu kwa mwaka ni Sh milioni 600 na hadi sasa ni vyama vya ushirika vitatu vimenufaika nao,” anasema Lyimo na kuongeza: “Vyama viwili vinatoka mkoani Katavi vikijihusisha na kilimo cha alizeti na kimoja kinatoka wilayani Karagwe katika Mkoa wa Kagera; kinachozalisha maharage,” anasema.
Hivyo, anasema mradi huo utaleta mabadiliko chanya kwa kuongeza uzalishaji na kukuza kipato kwa wakulima wadogo takriban 300,000. Aidha, utaimarisha biashara kwa kampuni ndogo 50 na vyama vya ushirika 30 ambavyo asilimia 25 vinaongozwa na wanawake na vijana. Kuhusu mradi maalumu wa mpango wa ajira kwa vijana unaolenga moja kwa moja vyama vya ushirika, Mratibu wa Shirika hilo hapa nchini, Mikidadi Waziri, anasema mpango huo umelenga kuvifikia vyama vya ushirika 20 nchini.
Waziri anasema katika awamu ya kwanza ya majaribio ya mradi, vyama saba vya ushirika kutoka Morogoro, Pwani, Ruvuma na Njombe vimepewa hundi yenye thamani ya Sh milioni 164.1. Vyama hivyo ni Chama cha Ushirika cha Umwagiliaji cha Ruvu (CHAURU ) kilipewa Sh milioni 34.6 na Chama cha Ushirika wa Wakulima Wadogo wa Kilimo cha Umwagiliaji Mpunga Dakawa, (UWAWAKUDA), Sh milioni 21.6.
Vingine na kiasi cha fedha katika mabano ni Chama cha IFCU ( Sh milioni 11), MAMCU (Sh milioni 36), TUCOCPRCOS ( Sh milioni 15.6), ISOWELU (Sh milioni 22.2) WINO SACCOS (Sh : milioni 12) na MAHANJE SACCOS (Sh milioni 11).
“Mradi huu maalumu umeweka masharti mepesi, chama lazima kiwe na ushirikiano na Agriterra na watakaoajiriwa wasizidi umri wa miaka 35 kwa maana vijana na Agriterra inachangia asilimia 75 na chama asilimia 25 kwa mwaka wa kwanza,” anasema Waziri.
Anasema mradi huo pia unatekelezwa katika nchi za Kenya, Rwanda, DRC -Congo, Zambia, Uganda na Sudan Kusini. Viongozi wa vyama vya ushirika akiwemo Mwenyekiti wa ISOWELU Amcos ya Njombe, Chesco Ng’eve, amepongeza Shirika kuanzisha mpango huo kwa kuwa utavinufaisha vyama kwa kuongeza uzalishaji wa mazao na kuviinua kiuchumi.
“Kwetu sisi, mradi huu maalumu utatunufaisha kiuchumi kwa wanachama tuliopo zaidi ya 420 tunaojihusisha na kilimo cha biashara cha viazi mvirigo katika eneo la ukubwa wa ekari zaidi ya 500,” anasema Ng’eve.