Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilimanjaro Express ruksa kuendelea na safari

Kilimanjaro (21).jpeg Kilimanjaro Express ruksa kuendelea na safari

Sun, 14 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) imeruhusu leseni na ratiba za mabasi 35 ya kampuni ya Kilimanjaro Truck Limited kuendelea kutumika baada ya kutimiza masharti.

Januari 6 mwaka huu, Latra ilitangaza kusitisha leseni na ratiba za mabasi 35 ya kampuni hiyo kuanzia Januari 8 baada ya kubainika kukiuka masharti ya leseni.

Miongoni mwa masharti hayo ni pamoja na kutoa huduma bila kutumia mfumo wa tiketi mtandao (e-tiketi) na kutoza nauli zaidi ya viwango vilivyoidhinishwa na Latra.

Taarifa iliyotolewa leo Jumapili Januari 15, 2024 na Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo imeeleza kuwa kampuni hiyo ilitakiwa kutekeleza masharti iliyopewa ikiwemo kutumia mfumo wa tiketi mtandao, kuzingatia viwango vya ukomo wa nauli pamoja na kuwasilisha maombi ya kurejesha huduma, ambayo yangeiwezesha mamlaka hiyo ya udhibiti kuhakiki mfumo wa tiketi mtandao.

"Baada ya kampuni kukamilisha maelekezo hayo ya Latra na kuwasilisha maombi ya kurejesha huduma, mamlaka kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani pamoja na Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Kumbukumbu (NIDC) imehakiki mfumo wa tiketi mtandao na nauli zilizoingizwa kwenye mfumo," amesema Suluo.

Amesema kupitia tangazo hilo mamlaka inawakumbusha watoa huduma wa mabasi yaendayo mikoani kuhakikisha mabasi yao yanabandikwa stika za madaraja kulingana na nauli husika na kuhakikisha hazitofautiani.

Aidha, Mkurugenzi huyo amesema kuna sehemu mfumo haukuunganishwa na Mamalaka ya Mapato Tanzania (TRA), hivyo hadi Februari mosi mwaka huu watoa huduma wote wanapaswa wawe wameunganishwa.

 "Si yeye tu, wapo na watoa huduma wengine ikifika hiyo tarehe hawajaunganishwa (na TRA) tutawazuia kutoa huduma, tunasubiri Serikali itupe nyenzo ya kuwadhibiti hawa kwa kuwa itakuwa imeshatoa kanuni," amesema Mkurugenzi huyo.

Hata hivyo, Suluo ameeleza kuwa mamlaka hiyo imekuwa ikitumika busara kwani kampuni hiyo imekuwa ikikiuka masharti mara kwa mara na kutozwa faini hadi kufikia Sh19 milioni ambazo wanaendelea kuzilipa.

Mwanasheria wa kampuni hiyo, Dickson Ngowi amesema wamekwishateleleza maelekezo waliyopewa, ikiwemo kuwa na tiketi mtandao zilizounganishwa na TRA.

Amebainisha kuwa magari yote yameshakaguliwa na kupewa tiketi za madaraja yanayohusika kuanzia daraja la chini hadi la juu.

 "Tunatoa angalizo kwa mamlaka zetu zinapochukua hatua, gari husika liwajibishwe kwa mujibu wa sheria badala ya kampuni nzima. Wapo wengine wanaokiuka lakini adhabu zao zinakuwa tofauti, busara zaidi itumike," amesema Ngowi.

Kwa upande wake mwakilishi wa Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (ZTO), Salum Morimori amesema maelekezo yaliyotolewa na sheria na taratibu vinapaswa kuzingatiwa kwa kuwa havipo kwa ajili ya mgogoro.

 "Kusimamisha leseni 35 hasa kwa kipindi hiki ni madhara makubwa, kwa kuwa sheria imeruhusu kutembea mchana na usiku, usalama unategemea pande zote mbili, busara itumile kwa wasafirishaji," amesema Morimori ambaye ni Mrakibu Mwanadamizi wa Polisi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live