Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilichobaki stendi ya Mwenge ni uzinduzi rasmi

Stand Mwenge .jpeg Kilichobaki stendi ya Mwenge ni uzinduzi rasmi

Tue, 12 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Uongozi wa Halmashauri ya Kinondoni umesema stendi ya Mwenge imeshafunguliwa na kilichobaki sasa ni uzinduzi rasmi, ambao utafanyika baada ya wafanyabiashara kumaliza kupanga bidhaa zao.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Machi 11, 2024 na Ofisa Biashara Mkuu wa halmashauri hiyo, Philipo Mwakibete, alipozungumzwa na waandishi wa habari kuhusu kinachoendelea katika stendi hiyo.

Stendi hiyo iliyoanza kujengwa mwaka 2019 na kugharimu zaidi ya Sh3 bilioni, ina jumla ya maduka 138 ambayo yalishachukuliwa yote tangu Novemba mwaka jana kwa njia ya mnada.

Akizungumza kinachoendelea kwa sasa, Mwakibete amesema kituo hicho kilianza kazi tangu Januari mwaka huu huku suala la uzinduzi likisubiri wafanyabiashara kumaliza kupanga bidhaa zao kwenye maduka waliyoyapangisha.

"Suala la biashara lina michakato yake, mtu anaweza kuchukua fremu, mzigo wa kuingiza akawa hana kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo labda mkopo aliotegemea kuupata kuweka bidhaa bado hajaupata au kuna marekebisho anayafanya kabla hajaweka vitu.

"Na sisi hatuwezi kumlazimisha mtu kama kachukua fremu leo aweke leo hiyohiyo tutakuwa hatujamtendea haki, japokuwa kodi yetu tunaendelea kukata vilevile tangu tulipoingia naye mkataba," amesema Mwakibete.

Aidha, amesema stendi hiyo inatarajiwa kuzinduliwa na kiongozi mkubwa hivyo ni muhimu wakati wa tukio hilo wafanyabiashara wakawa tayari wameshajipanga maeneo yao.

Katika hatua nyingine, Mwakibete amewaita wamiliki wa daladala kupeleka magari yao katika njia ya stendi hiyo.

Amesema daladala zinazotakiwa kuingia katika stendi hiyo ni 300 lakini mpaka sasa ni daladala 40 tu ndizo zilizojisajili .

"Katika kuleta daladala hapa hatutajali inatoka wilaya gani ilimradi tu uwe imekidhi vigezo na masharti yaliyowekwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri AĊ•dhini (Latra), hivyo anayeona gari lake lina sifa alete," amesema.

Wakati akiwa anaita daladala hizo kwa upande wao , madereva wa daladala zinazoishia safari zake Cocacola Mwenge wametaka nao waruhusiwe kuingia humo kwa kuwa wanapoegesha gari zao sio sehemu rafiki.

Mwenyekiti wa Umoja wa madereva, makondakta na wasimamizi wa daladala Mkoa wa Dar es Salaam (Umamadar), Juma Ombega, amesema awali wakati wanahamishwa kwa ajili ya ujenzi wa stendi hiyo waliambiwa walipo sasa watakaa kwa dharura na ujenzi ukiisha watarudi.

Ombega amesema cha ajabu wamekuja na masharti ya kutaka daladala zitakazoingia humo ziwe ni namba D na E na kuhoji matajiri wao wengine watapata wapi hela ya kununua magari mapya kwa sasa.

Akilijibu hilo Mwakibete amesema hayo yalikuwa ni maelekezo ya Latra kuwa namba hizo za gari mpya ndizo ambazo hazina ruti na wasingeweza kwenda kinyume na maelekezo yao.

Pia amesema vituo vya daladala vilivyowekwa ikiwemo cha Makumbusho na cha Coca havitahamishwa kwa sababu ya kukamilika kwa stendi hiyo kwa kuwa kote huko kuna mahitaji ya usafiri.

Hata hivyo, amesema katika kipindi hiki ambacho idadi ya daladala hazijatimia, wanaruhusu daladala zote zinazopita Mwenge kuingia kituoni hapo kushusha na kukupandisha abiria.

Katibu wa Umoja wa wamiliki wa daladala mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), Shifwaya Lema, amesema kuna mambo matatu yanayosababisha wamiliki kutopeleka magari huko ikiwemo vigezo vya namba.

Mmoja wa abiria aliyejitambulisha kwa jina la Tabia Mwakajeba, amesema kituo wamekipenda ni kizuri ila ombi lake na huduma zake ziwe nzuri ikiwemo magari ya njia zote yapatikane eneo hilo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live