Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kila soko Dar kuwa na fundi umeme anayetambulika Tanesco

Masoko Pic Data Makalla akiwa na Afisa Zimamoto

Fri, 29 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katika kukabiliana na majanga ya moto kwenye masoko ya Mkoa wa Dar es Salaam, kila soko litakuwa na fundi maalumu anayetambuliwa na Shirika la Umeme (Tanesco) atakayekuwa anahusika na kuangalia miundombinu ya umeme.

Maamuzi hayo yametolewa leo Ijumaa Aprili 29, 2022 na Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla katika kikao chake na viongozi wa masoko, wafanyabiashara na Jeshi la Zimamoto wa wilaya na Mkoa.

Makalla amesema amefikia maamuzi hayo baada ya kukithiri kwa majanga ya moto katika masoko ya mkoa huo ambapo akiwa hajamaliza hata mwaka mmoja tangu ateuliwe kuongoza Mkoa huo, masoko manne yameungua na kueleza kuwa sababu kubwa ukiangalia ni uzembe ikiwemo vishoka wanaotumika kuwaunganishia wafanyabiashara umeme.

Masoko yaliyoungua chini ya uongozi wake ni pamoja na Kariakoo, Cocacola, Mchikichini na Karume.

"Ifike mahali moto uwe basi kwenye masoko na kwa kuanzia ni kuondoa vishoka wa kuunganisha umeme kuweka mafaundi wanaotambulika na Tanesco, wakurugenzi, wakuu wa wilaya naomba mlizingatie hilo mara mnapotoka hapa," ameagiza Makalla.

Sambamba na hilo Mkuu huyo wa Mkoa ametaka kuwepo ukaribu kati Serikali na masoko na kueleza kusikitishwa kwake baadhi ya maofisa biashara hawajui baadhi ya masoko yalipo jambo linalodhiirisha nafasi waliyopo haiwatoshi na hawawezi kushughuliki changamoto zilizopo.

"Kama wafanyabiashara wanatoa ushuru kazi yetu Serikali ni kuhakikisha tunatoa huduma kwa masoko hayo na watendaji mna nafasi kubwa katika kuhakikisha hili linatekelezeka," amesema Makalla.

Wakati kuhusu suala la moto, amesema kuna haja ya kutolewa elimu ya mara kwa mara kwa wafanyabiashara wa masoko na kuwataka viongozi wao kuandaa ratiba ya namna bora ya kuweza kupatiwa elimu hiyo.

Katika kikao hicho, Jeshi la Zimamoto lilitoa elimu ya kujikinga na kukabilana na moto ambapo kupitia Sajenti wake Loyce Kibuta amesema asilimia 90 ya matukio ya moto yanatokana na wananchi wenyewe ikiwamo kuacha majiko yakiwaka au kujiunganishia umeme kiholela.

Awali wakiwasilisha changamoto zao baadhi ya wenyeviti wa masoko akiwemo soko la Mtongani, Hemed Panzi amesema Tanesco wasiwe wanapuuza wanapopewa taarifa za hitilafu za umeme jambo linalowafanya waamue kutumia vishoka ili kupata huduma hiyo kwa wepesi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wamachinga Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuph Namoto amesema kuna haja ya kuunda kikosi kazi kitakashowashirikisha Jeshi la Zimamoto na wamachinga ambao watasaidiana katika utoaji elimu ili kuwafikia wengi zaidi.

Kwa mujibu wa Makalla, Mkoa wa Dar es Salaam una jumla ya masoko 92 kati ya hayo masoko 70 ni ya Serikali na 12 ni ya binafsi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live