Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kila anayewekeza anatarajia faida, Serikali iwaamini matajiri

21329 Kila+pic TanzaniaWeb

Tue, 9 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Licha ya uhakika wa rasilimali za kufanikisha uzalishaji, kukosekana kwa uaminifu wa Serikali dhidi ya wafanyabiashara kumeelezwa kuwa ni kikwazo kitakachochelewesha au kukwamisha ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Tanzania inafaamika kwa wingi wa malighafi zinazohitaji kuongezewa thamani ili kukuza uchumi wa wananchi na pato la Taifa kwa ujumla kama vile madini, mifugo, misitu, maji ya kutosha na vyanzo vingi vya nishati.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), Subash Patel amesema kama kasumba ya Watanzania wengi kuhusu fedha na utajiri haitabadilika, Taifa litachelewa kufanikisha ndoto yake ya kuwa na uchumi wa kati mwaka 2025.

“Kila anayewekeza anatarajia (faida ya uwekezaji wake) return on investment. Changamoto iliyopo ni kumuona kila mwenye hela si mkweli. Haiwezekani uwekeze na usipate faida,” alisema Patel.

Alisema kutokana na hali hiyo, rasilimali zilizopo zinaendelea kubaki bila kutumika ipasavyo hivyo kuikosesha Serikali mapato mengi na wananchi wakiendelea kuishi kwenye ufukara.

“Ukiwa unanyeshewa mvua halafu ukaomba maji ya kunywa, hayo ni matatizo yako. Tunayo gesi lakini umeme unasuasua. Mafuta yamefika Dola 75 sasa hivi na huenda yakapanda mpaka Dola 90…wenye uwezo wa kutumia gesi waruhusiwe kuzalisha umeme,” alishauri.

Kutokana na kutoaminiana huko, mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye alisema kunaifanya Serikali itumie muda mwingi kutatua changamoto za viwanda vilivyopo badala ya kuweka mikakati ya kuanzisha vipya.

Simbeye alisema zipo sheria nyingi zinazoruhusu ubia kati ya Serikali na sekta binafsi lakini kutokana na upande mmoja kutouamini mwingine ndiko kunakofanya sheria hizo zisitekelezwe.

“(Kampuni ya Bia Tanzania) TBL wameingiza matenki lakini mpaka sasa yamekwama bandarini wanaambiwa wakiyasafirisha yataharibu barabara. Kuna vitu ukivisikia unashindwa kuelewa tatizo ni nini. Kwa hali hii naamini waziri natumia muda mwingi kusikiliza kero badala ya maoni ya namna ya kusonga mbele,” alisema Simbeye.

Aliishauri Serikali kuweka utaratibu wa kuwadhamini wajasiriamali kukopa fedha nyingi za kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwani nchini kuna changamoto ya upatikanaji.

Mkuu wa kitengo cha wateja wakubwa na Serikali wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi alisema fedha zinazohitajika kufanikisha uchumi wa viwanda ni nyingi kiasi cha kuzipa changamoto taasisi zilizopo kukidhi mahitaji hayo.

Alisema benki nyingi za ndani zinategemea amana za wateja hivyo inakuwa ngumu kwao kukopesha kwa muda mrefu kwani watashindwa kuzirejesha wenyewe watakapozihitaji.

“Tunapokopesha huwa tunaangalia maeneo yatayorudisha fedha ndani ya muda mfupi.

Viwanda vidogo

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema Serikali inajitahidi kuweka mazingira mazuri ya kuanzisha na kufanya biashara.

Mpaka sasa, alisema Tanzania inajitegemea kwa mahitaji ya chakula na bidhaa za ujenzi akitaja saruji, nondo na bati na msisitizo uliopo ni kujenga viwanda vitakavyotumia zaidi malighafi za ndani, vitakavyoajili watu wengi na sekta ya mafuta na gesi.

Mpango wa kuwa na uchumi wa kati kupitia viwanda ilianzishwa tangu mwaka 1997 ili kuboresha maisha ya wananchi.

“Miaka mitano ya kwanza mpaka 2011 ilikuwa ni kushughulikia vikwazo vya kufanya biashara. Tunaendelea vizuri na sasa tunao mwongozo wa kufanya biashara ambao utaanza kutumika muda si mrefu,” alisema waziri huyo.

Katika mpango huo, mpaka mwaka 2025 ingawa waziri alisema inaweza kuwa kabla ya hapo, kipato ch akila Mtanzania kinatarajiwa kuwa Dola 3,000 za Marekani kwa mwaka.

Katika mkakati wa kufanikisha lengo hilo, Mwijage alisema wajasiriamali wadogo wanahamasishwa kuanzisha viwanda vidogo vitakavyosaidi akuongeza thamani ya malighafi zinazowazunguka.

“Nchi nyingi zilizoendelea zinategemea viwanda vidogo, ukifikiria kiwanda kikubwa kama cha Wazo utakufa bila kukijenga kwa sababu wenye viwanda wengi mnaowaona walirithishwa na babu zao,” alisema Mwijage.

Mkurugenzi wa kampuni yaLindam Group, Zuhura Muro alisema hakuna haja ya kuiga uchumi wa viwanda uliojengwa katika nchi za magharibi kwani unaweza usifanye kazi ila muhimu ni kuangalia mazingira yaliyopo na kuyatumia ipasavyo.

“Watanzania wanategemea ardhi ambayo kwa dunia nzima inayofaa kwa kilimo, asilimia 60 ipo kusini mwa Jangwa la Sahara. Tuna maji mengi lakini hatujayatumii,” alisema.

Soko

Hata kama kila kaya itakuwa na kiwanda chake, wachokoza mada wa mdahalo huo wanaamini bidhaa zitakazozalishwa zitapata soko la kutosha endapo zitakuwa na viwango vinavyokubalika kwa wateja.

Mkurugenzi wa maendeleo ya biashara wa kampuni ya General Electric International Gilman Kasiga alisema Tanzania inapakana na nchi nyingi nane ambako bidhaa zote zinaweza kuuzwa kwa uhakika.

Si huko tu, alisema takriban watu milioni 60 waliopo nchini wanatoa soko la kutosha kwa wajasiriamali waliojipanga kulitumia likifuatiwa na la Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika (SADC).

“Kuna soko kubwa ndani hata kwa jirani zetu kama tutazichangamkia fursa zilizopo. Kujenga uchumi wa viwanda kutatuwezesha kukidhi mahitaji yetu na kuongeza pato la Taifa,” alisema Kasiga.

Chanzo: mwananchi.co.tz