Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kikokotoo kipya chapandisha pato la Taifa

42792 Pic+kikokotoo Kikokotoo kipya chapandisha pato la Taifa

Wed, 20 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Makadirio ya pato la Taifa kwa mwaka 2015 yaliyokuwa yakitolewa na taasisi za umma yalikuwa ni ya kiwango cha chini ikilinganishwa na hali halisi.

Hayo yamo kwenye ripoti mpya ya ukokotoaji wa pato la Taifa iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ambayo pamoja na mambo mengine, imetangaza kwamba kuanzia sasa ukokotoaji wa pato la Taifa na takwimu za uchumi utatumia bei za mwaka 2015 badala ya zile za 2007.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, pato halisi la Taifa kwa 2015 kwa kutumia bei za 2015 lilikuwa ni Sh94.3 trilioni badala ya Sh90.8 trilioni zilizokuwa zikikadiriwa kwa kutumia bei za 2007 ambalo ni ongezeko la asilimia 3.8.

Kwa mujibu wa bei mpya, kiwango cha shughuli za kilimo, misitu na uvuvi kilipungua hadi asilimia 26.7 mwaka 2015 ikilinganishwa na asilimia 26.8 kwa kutumia bei za 2007.

Ripoti hiyo inaonyesha upande wa mifugo, kiwango kilipungua hadi asilimia 7.6 mwaka 2015 kwa kutumia bei za mwaka 2015 kutoka asilimia 9.7 kwa bei za 2007.

Thamani ya kilimo, uvuvi, misitu ilifikia Sh25.2 trilioni kwa kutumia mwaka wa msingi 2015 kutoka Sh26 trilioni wakati wa kutumia mwaka wa 2007.

Hata hivyo, mchango wa sekta za viwanda na ujenzi iliongezeka hadi asilimia 24.5 katika mwaka mpya wa msingi, ikilinganishwa na asilimia 20.4 hapo awali.

Pato la sekta na ujenzi kwa mwaka 2015 lilipanda hadi kufikia Sh23.1 trilioni kwa kutumia bei za 2015 wakati wa kutumia bei za 2015, kutoka Sh21.8 trilioni wakati wa matumizi ya bei za mwaka 2007.

Huduma ziliendelea kuwa mchangiaji mkubwa kwa uchumi na asilimia 40.4 kwa kutumia bei ya 2015 kutoka asilimia 47.4 wakati wa kutumia bei za 2007.

Hata hivyo, ongezeko hilo ni dogo ikilinganishwa na la asilimia zaidi ya 30 lililopatikana wakati wa kubadilisha bei kutoka mwaka 2001 hadi 2007.

Hatua hiyo imeshusha kiwango cha ukuaji wa uchumi hadi asilimia 6.3 mwaka 2015 kwa kutumia bei za mwaka 2015 kutoka asilimia zaidi ya saba kwa kutumia bei za mwaka 2007.

Pamoja na kushuka kwa ukuaji wa uchumi, pato kwa kila Mtanzania lilifikia Sh2.3 milioni kwa mwaka 2017, hali inayoashiria kuanza kwa safari ya kuelekea uchumi wa kipato cha kati miaka sita ijayo.

Miaka sita iliyopita, pato la kila Mtanzania lilikuwa ni Sh1.6 milioni. Hii ilikuwa ya chini kuliko upanuzi wa asilimia 32 iliyoandikwa wakati wa marekebisho ya awali uliofanyika mwaka 2013 ili kubadilisha mwaka wa msingi tangu 2001 hadi 2007.

Mwaka 2013 baada ya kupitishwa kwa mwaka wa bei mpya ya 2007, pato la Taifa lilikuwa Sh69.8 bilioni, kutoka kwenye makadirio ya awali ya Sh53 trilioni.

Mkurugenzi wa Takwimu za Kiuchumi wa NBS, Daniel Masolwa aliliambia Mwanachi kuwa maboresho hayo yalizingatia uingizwaji wa sekta mpya ambazo zilikuwa haziingizwi kwenye ukokotoaji wa pato la Taifa.

Alisema pato la Taifa limeboresha uchumi kwa sababu kuna ongezeko la shughuli za kiuchumi ambazo awali hazikujumuishwa kwenye takwimu za kiuchumi.

“Miaka 10 iliyopita, watu walikuwa wakitumia telegramu kutuma pesa, lakini huduma za fedha za simu za mkononi imekuwa shughuli mpya ya kiuchumi ambayo imechangia kuongezeka kwa ajira na kodi,” alisema.

Alisema maendeleo haya ya ukuaji wa pato la Taifa, hayataathiri moja kwa moja maisha ya Watanzania lakini ni kichocheo cha kuboresha shughuli za kiuchumi.

Alisema wakati mkulima akivuna mazao yake na akaamua kuweka mapato ya uzalishaji chini ya kitanda, huwezi kuona mabadiliko kwenye maisha yake.

Mkurugenzi wa utafiti wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na mkurugenzi wa utafiti wa uchumi na sera, Dk Suleiman Misango walisema mapitio hayo yanatokana na kupitwa na wakati kwa matumizi ya bei za mwaka 2007.

Chanzo: mwananchi.co.tz