Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kijaji aagiza maofisa biashara kusimamia bei za bidhaa

Dkt Kijaji Maofisa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji

Tue, 25 Jul 2023 Chanzo: Mwananchi

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji amewaagiza maofisa biashara waliopo kwenye halmashauri, kuhakikisha wanasimamia bei ya bidhaa ipasavyo, ili kuepuka upandishaji holela.

Dk Kijaji ameyasema hayo leo Jumanne Julai 25, 2023 wakati akielezea mwenendo wa bei za bidhaa nchini.

Amewataka wazalishaji viwandani kuongeza jitihada za uzalishaji wa bidhaa kwa ubora unaohitajika sokoni, na kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa, ili kukabiliana na kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali nchini.

“Hatutovumilia kuona mzalishaji, msambazaji au muuzaji wa bidhaa yoyote ile, akiongeza kiholela bei ya bidhaa bila sababu ya msingi,” amesema.

Aidha, amesema bei ya saruji (aina ya 32.5) kwa Julai 2023 ni kati ya Sh 14,125 na Sh23, 250 kwa mfuko wa kilo 50, huku bei ya juu ya saruji hiyo imeongezeka kwa asilimia 0.5.

Amesema ongezeko la bei ya juu kwa bidhaa hiyo ni sawa na Sh125 kwa mfuko wa kilo 50, ikilinganishwa na bei ya Juni 2023 ambayo ilikuwa ni Sh23, 125 kwa mfuko wa kilo 50.

Amesema bei ya chini ya saruji imeongezeka kwa asilimia 4.6 sawa na ongezeko la Sh625 kwa mfuko wa kilo 50 ikilinganishwa na bei ya Juni 2023 ambayo ilikuwa ni Sh13,500 kwa mfuko wa kilo 50.

Aidha, amesema uchambuzi wa wastani wa bei ya saruji (aina ya 32.5) nchini unaonesha kuwa bei yake imepanda kwa asilimia 3.2 ukilinganisha na wastani wa bei ya bidhaa hiyo kwa Juni 2023.

Amesema mkoa wenye bei ya chini ni Tanga, wakati bei ya juu ipo katika mkoa wa Kagera.

Dk Kijaji amesema ongezeko hilo linatokana na kuongezwa kwa ushuru wa Sh20 kwa kila kilo ya saruji kutoka mwaka wa fedha 2023/24.

Kwa ongezeko hilo, mfuko mmoja wa saruji wenye kilo 50 umeongezeka Sh1, 000.

Chanzo: Mwananchi