Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kigwangalla ataka kampuni za utalii kutumia wageni kuitangaza Tanzania

9998 Pic+kigwangala TanzaniaWeb

Sat, 4 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla ameyataka makampuni yanayopokea watalii kushirikiana na Serikali kuitangaza nchi.

Amesema kampuni hizo zinaweza kuitangaza Tanzania kupitia wageni maarufu wanaowapokea.

Akizungumza leo Ijumaa Agosti 3, 2018 katika kikao cha kuelezea mchakato wa kupatikana utambulisho mpya wa utalii nchini, Dk Kigwangalla amesema ni muhimu ukawepo ushirikiano wa wadau mbalimbali kuitangaza Tanzania.

Amesema watu hao maarufu wanaweza kutumika kuitangaza nchi ikiwa watawaomba licha ya kubainisha kuwa baadhi ya wageni huweka usiri kuhusu uwepo wao nchini.

Miongoni mwa watu maarufu waliotembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini hivi karibuni ni pamoja na rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama na Rais wa Uswisi, Iaun Berset, wote wakiwa wameambatana na familia zao.

Kuhusu mchakato wa kupata utambulisho wa utalii wa Tanzania, amesema umekwenda vizuri na baada ya utafiti jina lililopendekezwa ni Tanzania unforgettable.

Amesema Rais John Magufuli anatarajiwa kuzindua rasmi utambulisho huo wa utalii wa Tanzania, ambao utaambatana na picha itakayowakumbusha watalii duniani kote kuhusu Tanzania.

Awali, Mkurugenzi wa Bodi ya Taifa ya Utalii (TTB), Devota Mdachi amesema mchakato wa kupata utambulisho umefanywa na kamati ya wajumbe 21 iliyoundwa na waziri huyo.

Amesema katika mchakato huo watu 651 waliohojiwa kutoka mataifa 54 na kusaidia kupata utambulisho Tanzania unforgettable.

"Awali utambulisho wetu ulikuwa ni Tanzania the land of Kilimanjaro, Serengeti and Zanzibar lakini tukaona kuna vivutio vingine havitajwi,” amesema.

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro na mkuu wa wilaya ya Arumeru ni baadhi ya viongozi waliohudhuria.

Chanzo: mwananchi.co.tz