Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kicheko wakulima kahawa kunufaika mashine za uchakataji

Kahawa Pc Kicheko wakulima kahawa kunufaika mashine za uchakataji

Mon, 6 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakulima wa kahawa kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Mbinga na Songwe wameanza kunufaika na matumizi ya teknolojia ya mashine ya kisasa kuchakata zao hilo ndani ya muda mfupi.

Mashine hizo ambazo zimeanza kuingizwa kutoka nchini Colombia zina uwezo wa kuchakata zao hilo kuanzia kilo 300 mpaka 20,000 kwa saa moja.

Akizungumza na Mwananchi, meneja wa kampuni ya JM Estrada kutoka Medellin nchini Colombia, Sandra Cardenas, amesema wameingiza teknokojia hiyo baada ya kubaini kuwepo kwa changamoto kwa wakulima kuzalisha kwa ubora, kuchataka, kuondoa maganda na sukari ambapo inasababisha kukosa sifa.

Cardenas aliyasema hayo kwenye banda la maonyesho la kampuni hiyo ikiwa ni Maadhimisho ya Siku ya Kahawa Duniani yaliyofanyika katika Kiwanda cha Kukoboa Kahawa Mbozi (MCCCO) Mkoa wa Songwe.

“Matumizi ya teknolojia hiyo imeleta mapinduzi makubwa kwa wakulima waliojiunga kwenye vyama vya msingi vya wakulima (Amcos) na kuweza kubadili mifumo ya maisha kupitia zao hilo,” amesema

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni hiyo Ulf Kusserow, amesema ni wakati sasa wakulima kutumia fursa hiyo katika kilimo biashara ili kupanua wigo wa kiuchumi na kuchangia mapato Serikali.

“Lengo ni kuona tunawekeza zaidi kwenye sehemu ya kuchakata, pia kulinda uchafuzi wa mazingira kwa kuwajengea miundombinu rafiki kwa wenye mahitaji ya kufungiwa majumbani au kwenye Amcos sambamba na kuwaonganisha na Taasisi a kifedha” amesema.

Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Moses Simwinga amesema teknolojia hiyo itakuwa mkombozi kwa wakulima hususan waliojiunga kwenye Amcos.

Kadhalika, Meneja wa kituo cha Utafiti wa Kahawa (Tacri) Dismas Pangaras amesema kwa kushirikiana na wadau wanaendelea kuboresha kilimo cha kahawa nchini ili kufikia malengo waliyokusudia ifikapo 2025.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa amepongeza nchi ya Colombia kwa kubuni teknolojia hiyo ambayo inakwenda kumsaidia mkulima wa chini kujikwamua kiuchumi kwa kutotumia nguvu kubwa katika uchakataji.

Mkulima wa kahawa Mwajuma Ally, amesema uwepo wa teknolojia ya mashine hizo kumekuwa mkombozi mkubwa kwa wakulima kwani kwa sasa wamekuwa wakizalisha kwa ubora mkubwa na bei nzuri.

“Kimsingi tuna kila sababu ya kushukuru kwani tumetumia nguvu kubwa kuvuna kidogo lakini sasa tunapata kikubwa sambamba na uondoaji wa sukari kwa ubora wa kiwango kinachotakiwa katika soko.”amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live