Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kicheko Ziwa Tanganyika likifunguliwa upya

Ziwa Tanganyikauvuvi.jpeg Kicheko Ziwa Tanganyika likifunguliwa upya

Fri, 16 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imelifungua rasmi Ziwa Tanganyika baada ya kufungwa kwa kipindi cha miezi mitatu tangu Mei 15, 2024 huku ikikemea uvuvi haramu unaosababisha upungufu wa mazao ya uvuvi ziwani humo.

Serikali ilisitisha shughuli za uvuvi katika ziwa hilo linalozungukwa mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa hadi Agosti 15, 2024 ili kuruhusu samaki kuzaliana na kuongeza tija kwa wavuvi wanaofanya shughuli zao ziwani humo.

Akizungumza jana Alhamisi, Agosti 15,2024 Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema ni muhimu wavuvi kutunza ziwa hilo kwa ajili yao na vizazi vijavyo.

Amesema Serikali inatumia gharama kubwa kuzuia uvuvi haramu na kwamba Serikali itawachukulia hatua wavuvi wote watakaokuwa wanaojihusisha na uvuvi haramu.

“Serikali inafanya yote haya na kusitisha shughuli za uvuvi kwa muda si kuwakomoa wananchi wake kwani tunafuata mchakato wote kutoka kwa wataalamu wetu waliofanya utafiti na hatukurupuki kufanya maamuzi,” amesema Waziri Ulega.

Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Salum Kalli amepiga marufuku watu watakaojihusisha na ulanguzi wa mazao ya uvuvi katika ziwa hilo na kutaka watu wanunue kwa bei za kawaida zinazojulikana kila siku.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Edwin Mhede amesema ni muhimu kulinda rasilimali za uvuvi kwa kuwa asilimia 10 ya Watanzania wapo kwenye sekta hiyo.

Baadhi ya wavuvi wa Ziwa Tanganyika wakijiandaa kuingia ziwani kuvua samaki na dagaa ikiwa ni baada ya miezi mitatu tangu kufungwa kwa ziwa hilo Mei 15,2024.

Amesema kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2024 iliyofanyika ukanda wa Ziwa Tanganyika inaonyesha kuwa kuna wavuvi wapatao 32,757 ukilinganisha wavuvi 29,571 waliokuwepo kwenye matokeo ya sensa ya wavuvi waliokuwepo mwaka 2022.

Kuhusu mazao ya uvuvi, Mhede amesema mwaka 2023 zilipatikana tani 479,000 za samaki kwa nchi nzima sawa na Sh3.4 trioni na kati ya hizo tani 85 sawa na asilimia 17 zenye thamani ya Sh613 bilioni zilitoka katika Ziwa Tanganyika.

Baadhi ya wavuvi wa mwalo wa Katonga, wamesema kufunguliwa kwa ziwa hilo wanategemea kupata samaki na dagaa za kutosha na kwamba watatoa ushirikiano kwa Serikali dhidi ya uvuvi haramu.

Kido Jamal amesema walikuwa wanasubiria kwa hamu kuingia ziwani na kupata samaki kwani wameteseka kwa muda mrefu bila kula mgebuka wala dagaa.

“Tulikuwa na hali ngumu sana ya maisha, binafsi nilikuwa nategemea ziwa hili kulisha familia yangu na mahitaji muhimu, hivyo kufunguliwa kwa ziwa kunatupa unafuu kwa maisha kwa kupata mahitaji ya familia yangu,” amesema Richard Hussein.

Uamuzi wa Tanzania wa kusitisha shughuli za uvuvi katika Ziwa Tanganyika ulitokana makubaliano kwenye kikao kilichofanyika mwaka 2022 kikihusisha nchi zinazozunguka ziwa hilo – Zambia, Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Uamuzi huo ni utekelezaji wa mkataba wa kikanda wa nchi wanachama wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika unaoweka hatua na taratibu za usimamizi endelevu wa shughuli za uvuvi katika ziwa hilo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live