Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kibano chaja kwa wamiliki wa matrekta

Trekta Siku 7 Kibano chaja kwa wamiliki wa matrekta

Fri, 20 Sep 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ameagiza kuandikishwa kwa wafanyabiashara binafsi wanaotoa huduma za kuwalimia wakulima kwa matrekta ili kuboresha ufuatiliaji wa huduma zinazotolewa kwa wakulima nchini.

Usajili huo pia unalenga kuanzisha njia za kuwafanya walipe kodi katikati ya shutuma za kuwatoza wakulima gharama kubwa wakulima huku wenyewe wakikusanya fedha pasipo kulipa kodi.

Bashe alitoa maelekezo hayo Alhamisi, Septemba 19, 2024, katika Wilaya ya Madaba, Mkoa wa Ruvuma, wakati wa ziara yake inayoendela mkoani humo.

Akizungumza baada ya kukagua kituo cha ununuzi wa mahindi cha Mtyangimbole na Madaba wilayani humo, Bashe amesema Serikali imejizatiti kubadilisha kilimo nchini kupitia ongezeko la matumizi ya teknolojia ya kilimo, hasa matumizi ya zana bora za kilimo.

Hata hivyo, amesema juhudi za Serikali zimekabiliwa na changamoto kutoka kwa wafanyabiashara binafsi ambao wamekuwa wakiwatoza wakulima gharama kubwa wanapokodi matrekta, hivyo kuwaongezea kwa gharama za uzalishaji.

"Peramiho, wakulima wanalipa hadi Sh120,000 kwa ekari. Vilevile, hapa Madaba, gharama za kukodi trekta zinaanzia Sh80,000 hadi Sh120,000, ambayo ni kubwa sana kwa wakulima," aliwambia wakulima katika mkutano huo.

"Gharama hizi zimekuwa zikiongezeka sana na kuathiri shughuli za wakulima, na kusababisha kushindwa kupata manufaa waliyotarajia kuathari uwekezaji na kujitolea kwao katika sekta hiyo," ameongeza.

Amesema usajili wa watoa huduma hizo utawezesha wizara kufuatilia kwa karibu na kulinda maslahi ya wakulima na, muhimu zaidi, kuwaingiza miongoni mwa watu wanaostahili kulipa kodi.

"Hivyo basi, kila mtu anayeshughulika na utoaji wa huduma hizo wapataswa kuandikishwa na kulipa kodi kwa sababu wanachokifanya ni biashara," aliwaeleza wakulima wilayani humo.

Bashe amesema Serikali ina mpango wa kununua trekta 10,000 ifikapo mwaka 2030, akibainisha kwamba zitagawanywa katika vituo mbalimbali vya utoaji huduma ambapo wakulima watapata huduma kwa bei ya ruzuku.

"Kituo cha utoaji huduma hizo kitajengwa katika Kijiji cha Ngadinda. Kitakapoanza kazi, gharama za kukodi trekta zitashuka hadi Sh40,000," alisema.

Waziri Bashe amesema utafiti umeonyesha kuwa wafanyabiashara wanaweza kupata faida kwa kutoza kati ya Sh35,000 na Sh40,000 kwa ekari.

Zaidi ya hayo, amesema katika vituo hivyo, wakulima watapatiwa huduma nyingine ikiwemo utafiti wa udongo, usambazaji wa mbolea, ununuzi wa mbegu, na ushauri katika sekta ya umwagiliaji.

Amesema huduma hizo zitakazotolewa kwa ruzuku ni muendelezo wa juhudi za serikali za kupunguza gharama za uzalishaji zinazotolewa kwa wakulima.

"Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ulianza kwa kuidhinisha utoaji wa mbolea kwa ruzuku. Baadae huduma hizo zilipanuliwa hadi utolewaji wa mbegu za mazao za ruzuku kuanzia msimu huu hususani mbegu za mahindi ambazo zitasambazwa kwa ruzuku kuanzia msimu huu," alisema.

"Utambulisho wa ruzuku katika huduma za matumizi ya zana za kilimo utapunguza gharama zinazowakabili wakulima. Ruzuku hizi zote zitaendelea katika miaka miwili ijayo hadi wakati ambapo uwezo wa wakulima kushiriki kwa ushindani sokoni utakapojengwa kikamilifu," ameongeza Bashe.

Mkulima na mkazi wa Kijiji cha Mahanje, Theresia Luambano, amesifu uamuzi wa Serikali wa kuwasajili watoa huduma wa zana za kilimo, akisema kuwa hatua hiyo ni ukombozi kwa kilimo nchini.

"Uamuzi huu utaondoa mzigo wa wakulima kulipa Sh80,000 hadi Sh120,000 kwa trekta kwa ekari. Mpango huu utabadilisha mitazamo ya wakulima na kuwafanya waanze kufikiria kupanua mashamba yao," amesema.

Mkulima mwingine na mkazi wa Kijiji cha Madaba, Cotas Mbilinyi, alikubaliana na Luambano, akisema ni wakati muafaka kwa watoa huduma za zana za kilimo eneo hilo kulipa kodi kama wakulima binafsi.

"Tunahitaji kujenga Taifa lenye usawa ambapo kila mtu analipa kodi na kusaidia maendeleo ya kiuchumi nchini badala ya kuliacha jukumu hilo kwa watu wachache. Wakati wakulima wengi masikini wanatozwa kodi, wachezaji hawa wamekuwa wakijikusanyia na kufaidi mapato yanayotokana na biashara hiyo pasipo kulipa kodi," alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live