Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kibano cha TRA kodi ya pango

Kodi Pango Tra Kibano cha TRA kodi ya pango

Sun, 14 Aug 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

akati Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikitangaza mikakati itakayoiwezesha kukusanya zaidi Sh23.65 trilioni ndani ya mwaka wa fedha wa 2022/23, ukiwamo mpango wa kutoza kodi kwa wamiliki wa nyumba za kupanga, wamiliki na wapangaji hao, wamelalamika kuwa hatua hiyo inazidi kuwaongezea makali ya maisha.

Hatua hiyo ya TRA inakuja wakati tayari Serikali imeshaanza kutekeleza mkakati mwingine wa kukata kodi ya majengo, inayotozwa kupitia mfumo wa ununuzi wa umeme wa Luku.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini hapa, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa kodi, Richard Kayombo alisema hatua hiyo inatokana na marekebisho ya Sheria ya Kodi, inayowapa mamlaka wapangaji kuzuia kodi ya pango ya asilimia 10 katika nyumba binafsi na za kibiashara na kisha kuiwasilisha TRA ili kurahisisha ulipaji na ukusanyaji wa kodi ya pango.

Kodi hiyo itawasilishwa na mmiliki wa nyumba kwa TRA, japo hata mpangaji anaweza kuikata moja kwa moja na kuiwasilisha.

“Tunaweka utaratibu mzuri ambao ukikamilika tutatoa taarifa ambayo tutashirikisha serikali za mitaa, watendaji na wilaya,” alisema Kayombo.

Alisema ukusanyaji huo wa kodi ya pango la nyumba ni sehemu ya mikakati ya makusanyo ya bajeti ya Serikali ya Sh41.48 trilioni.

Alisema kwa mwaka wa fedha uliopita 2021/22, TRA ilikusanya kiasi cha Sh 22.9 trilioni na kufikia lengo la asilimia 99.22, ambao ni ukuaji wa asilimia 22.77.

Hata hivyo, mkakati huu sio mpya na kinachofanyika kwa TRA ni kuja na mpango mkakati wa kuhakikisha inakusanya mapato hayo kwa ufanisi zaidi.

Awali asilimia hiyo haikuwa ikipelekwa TRA, hivyo wapangaji kulipa kiasi chote cha pango kwa wamiliki wa nyumba, sambamba na wapangaji hao kulipa pango la mwezi mmoja kwa dalali aliyetafuta nyumba.

Mchumi atahadharisha

Akizungumzia hatua hiyo, mchambuzi wa masuala ya uchumi, Dk Abel Kinyondo alisema japo Serikali inalenga kuongeza mapato, inaweza kuingia hasara zaidi.

Alisema ukimnyonya sana ng’ombe atatoa maziwa, lakini kuna wakati atafika ataanza kutoa damu, na mwisho akifa hata kile kidogo kilichokuwa kinapatikana mtu unakikosa.

“Sisi tunachowaza ni kuamka na kuongeza kodi, lakini hatujawahi kukaa kuwaza ni kwa nini tusiweke mazingira bora ya ufanyaji wa biashara yakawepo mazingira bora ya watu kuwekeza kwenye viwanda, ili vitakapokuwa vingi tuwe na sehemu ya kukata kodi,” alisema Dk Kinyondo.

Alisema moja ya misingi ya utozaji kodi ni kutotoza kodi kupita kiasi, bali kuongeza wigo wa kodi.

Alibainisha kuwa kuongeza wigo wa kodi ni kuhakikisha kuna mazingira mazuri ya ufanyaji biashara, ili kila siku aweze kutokea mlipa kodi mpya ambaye hakuwepo.

“Kinachotokea sasa hivi kila siku inapangwa kodi mpya ya kumtoza mtu yuleyule, unakuwa hujaongeza wigo wa kodi kwa kutengeneza mazingira mazuri ya kibiashara ili kila wakati aongezeke mtu au biashara,” alisema.

Wanachosema wapangaji, wenye nyumba

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi, baadhi ya wapangaji walisema hatua hiyo inaongeza maumivu kwao.

“Mpangaji anapopata nyumba anatakiwa kumlipa dalali aliyemsaidia kodi ya mwezi, alipe kodi kwa mwenye nyumba, tunaponunua umeme tunakatwa kodi ya majengo, bado malipo mengine kama bili za maji, taka na ulinzi shirikishi ni maumivu kwa kweli,” alisema Hajira Msami, mkazi wa jijini hapa.

Kwa upande wake James Mashauri, mkazi wa Tabata Segerea alisema japokuwa kodi hiyo inalipwa na wenye nyumba, lakini inaweza kuongeza kodi kwa wapangaji na hivyo kuongeza mzigo.

Hivyo aliiomba Serikali kuangalia namna ya kuwadhibiti wenye nyumba wasiongeze kiasi cha kodi wanacholipwa na wapangaji.

“Serikali isipokuja na mbinu ya kuwadhibiti wenye nyumba katika uongezaji wa kodi kwa wapangaji, kodi hiyo itazidi kuongeza makali ya maisha kwa wapangaji,” alisema.

Naye Hassan Abdallah, mkazi wa Kibaha alishauri kwanza kabla ya kuanza kuchukuliwa kwa kodi hizo, ni vyema wangeanza kwa kutengeneza mfumo mzuri wa utambuzi wa nyumba kwa ajili ya makazi binafsi na zile zinazopangishwa.

“Sidhani kama kuna mfumo rasmi wa kutambua nyumba za kupanga na zile binafsi, hivyo ni vyema kuanza kufanya utambuzi wa nyumba hizo kabla ya kuanza kazi kwa kodi hiyo,” alisema.

Serikali za Mitaa

Wakati Serikali ikitangaza mkakati huo, baadhi ya wenyekiti wa serikali za mitaa wamesema hawana taarifa kuhusu suala hilo, kwani ndio kwanza wanalisikia.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Nyakwale, Kata ya Kibada jijini hapa, Said Shomari alisema kuna haja ya kushirikishwa kwa karibu, ikiwemo mikataba ya wapangaji na mwenye nyumba iwe lazima kupitia serikali ya mtaa.

“Tutakapopata elimu sisi wenyeviti nini TRA inataka kufanya katika hilo, nasi tutatumia mikutano yetu ambayo kisheria tunapaswa kuifanya kila mwezi mara mbili na wananchi kuwaelimisha mambo haya, ili kusiwe na mikwaruzano katika kukusanya kodi hiyo.

“Nadhani ni wakati sasa TRA ikafika kwa mkurugenzi wa halmashauri ambaye naye atatoa maelekezo kwetu ya kuwepo kwa fomu hizo, ambazo naamini ikiwa hivyo Serikali itakusanya kodi hizo kirahisi,” alisema Shomari.

Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Serikali za Mtaa jijini Dar es Salaam, Juma Mwingamno alisema TRA wasichukulie jambo hilo kirahisi, ukizingatia asilimia 70 ya wakazi wa majiji mengi ni wapangaji, huku 30 iliyobaki ndio wenye nyumba.

Mwenyekiti Serikali ya Mtaa wa Ngobedi, Kata ya Chanika, Mohamedi Kilungi, naye anaungana na wa Nyakwale kuwa hana taarifa hiyo, kwani ndio kwanza anaisikia.

“Hawa watu wamekuwa wakipanga baadhi ya mambo yao bila kutushirikisha wakati wanajua sisi ndio tupo huku chini na wananchi, ukweli ni kwamba jambo hili nalisikia kwako leo,” alisema.

Madalali watoa neno

Kwa upande wake, dalali Joseph Shemdoe, anayefanya shughuli zake maeneo ya Kinondoni, alisema hatua hiyo ya Serikali kukusanya kodi ni nzuri, lakini wasiwasi wake ni kwamba mzigo huu utaenda kumwangukia mpangaji.

Naye dalali James Shirima anayefanya shughuli zake maeneo ya Buguruni, alisema hilo ni jambo zuri kama kutawekwa mfumo mzuri wa kubaini nyumba zinazopangishwa, tofauti na sasa hivi biashara hiyo hufanywa kati ya mwenye nyumba na mpangaji.

Alipoulizwa haoni kama na wao itabidi washiriki katika utoaji kodi hiyo, alisema ni ngumu kutokana na mateso wanayoyapata wakati wa kuwatafutia wapangaji nyumba, hivyo hilo ni vyema mwenye nyumba na mpangaji wake wakalimaliza wenyewe.

“Yaani hapa tutegemee chumba kilichokuwa kikipangishwa kwa mfano Sh100,000 kitapanda na kufika Sh120,000 hadi 130,000, mwenye nyumba hawezi kukubali hela yote ya kodi ailipe mwenyewe,” alisema Shirima.

Lukuvi na madalali

Novemba 26, 2021, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alipiga marufuku madalali wa nyumba kutoza fedha sawa na kodi ya mwezi mmoja kwa wapangaji pindi wanapotafuta makazi au maeneo ya biashara.

Kwa muda mrefu madalali wamekuwa wakitoza fedha sawa na malipo ya mwezi mmoja ama kutoka kwa wapangaji, wenye nyumba au kotekote.

Hata hivyo, Lukuvi ambaye hakusema ni kiasi gani madalali wanatakiwa kulipwa au utaratibu upi utumike, alisema huo ni wizi kama wizi mwingine.

Alisema hakuwahi kulijua jambo hilo hadi lilipoibuka kwenye mjadala kuhusu madalali wanaowaumiza wakulima, wanunuzi na wawekezaji kwenye sekta ya misitu.

“Hawa wanaochukua kodi ya mwezi mmoja ni majambazi, wizi huu ukome na ni marufuku mpangaji kumlipa dalali. Watasema itawezekanaje, wao waendelee tu na wananchi wengi wanayo namba yangu. “Mimi nakomesha jambo hili, na tulishasema kodi ni ya mwezi mmojammoja si miezi 12. Fikiria mtu analipa kodi ya miezi 12 halafu anamlipa dalali mwezi mmoja, yaani miezi 13 ni mwaka gani una miezi 13?”

Hata hivyo, kauli hiyo ya Lukuvi iliwaibua madalali ambao walisema hiyo ni kazi kama nyingine na kuwataka wapangaji wanaotafuta nyumba kumpigia waziri huyo awasaidie kupata makazi.

Desemba 15, 2021, katika kudhibiti na kusimamia kazi za udalali wa upangishaji na uuzaji wa nyumba, viwanja na mashamba nchini, Serikali iliagiza madalali kuwa na vitambulisho na vyeti maalumu vya kufanya kazi hiyo.

Pia, ilisema kuwa madalali hao watapaswa kuwa na leseni itakayokuwa na taarifa ya mlipa kodi, huku wale wa kampuni kutakiwa kuwa na mashine za kulipa kodi.

Makubaliano hayo yalifikiwa kwenye kikao cha Lukuvi na madalali ambapo, kila dalali atapaswa kulipia Sh20,000 kwa mwaka, na vitakuwa vinapatikana katika halmashauri zote nchini, huku cheti kikiwa kinamhalalisha kufanya kazi hiyo.

Mikakati mingine

Kwa upande mwingine, Kayombo alitaja mikakati mingine ya kuongeza ukusanyaji wa mapato kuwa pamoja na kuimarisha mifumo iliyopo na kuzindua mipya ya kukusanya kodi mbalimbali ili kuongeza ufanisi, urahisi wa ulipaji, ukusanyaji pamoja na kuokoa muda na gharama kwa mlipakodi na TRA.

Kayombo alisema ili waweze kufikisha lengo la kukusanya Sh23.65 trilioni, wamejipanga kuongeza usimamizi wa utoaji kwa njia ya mashine za risiti za kielektroniki (EFD) pamoja na kuziba mianya mbalimbali ya udanganyifu.

Alitolea mfano kuna mtu anapoenda kununua bidhaa anaambiwa akikatiwa risiti bei inakuwa kubwa, lakini bila risiti bei inakuwa ndogo, hivyo watahakikisha wanatoa elimu ili mwananchi aelewe umuhimu wa kudai risiti pindi anaponunua bidhaa.

Alisema pia maboresho ya Sheria ya kodi yanarahisisha ulipaji kodi kwa wafanyabiashara wadogo wenye mauzo kati ya Sh11 milioni hadi Sh 99.9 milioni kuwa na kiwango cha asilimia 3.5 ya mauzo ili kurahisisha utozaji kodi.

Imeandikwa na Pamela Chilongola, Mariam Mbwana, Nasra Abdallah na Fortune Francis.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz