Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kauli ya NEMC kwa viwanda vinavyozalisha vinywaji vya kuchangamsha mwili

Energy Drink Glass (600 X 313) Kauli ya NEMC kwa viwanda vinavyozalisha vinywaji vya kuchangamsha mwili

Tue, 7 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limevitaka viwanda vinavyotumia chupa za rangi kuweka kinywaji cha kuchangamsha mwili kuhakikisha wanaweka utaratibu wa kuzirejeleza chupa hizo.

Baraza hilo limesema kuna viwanda vinatumia chupa hizo, lakini havijaweka utaratibu wa kuhakikisha baada ya matumizi ya yake mazingira yanasafishwa.

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Samuel Gwamaka ameeleza hayo leo leo Jumanne Novemba 7, 2023 wakati akizungumza na wanahabari kuhusu hatua mbalimbali za kukabiliana na uwepo wa chupa hizo.

“NEMC tunatoa tamko la kuwataka wenye viwanda vinavyotumia chupa za rangi kuwa na mitambo au utaratibu wa kuzirejeleza baada ya matumizi."

“Pale ambapo hakuna utaratibu wa kurejeleza hizi chupa wala kuzikusanya chupa kutoka katika mazingira, basi tunawapa mwezi mmoja wa kufanya maboresho na marekebisho kuhusu suala hili ambalo ni takwa la kisheria,” amesema Dk Gwamaka.

Amesema NEMC ikianza ukaguzi utakaoanza baada ya mwezi mmoja kwa wazalishaji wa vinywaji hivyo vinavyotumiwa chupa za rangi na kugundua katika mitambo yao hakuna utaratibu wa kuzikusanya wala miundombinu ya kuzirejeleza hatua za kisheria zitachukuliwa.

“Tutachukua hatua ya kukifunga kitengo cha kinachotumika kuzalisha vinyawaji hadi pale wahusika watakapoweka utaratibu uliolekezwe na baraza hili,” amesema Dk Gwamaka.

Dk Gwamaka amesema miaka ya nyumba NEMC ilikutana na wazalishaji wa bidhaa hizo na kuwapa semina kuhusu wajibu wao wanaotakiwa kuufanya katika shughuli hizo hili kulinda mazingira yanayotoka na uwepo wa chupa hizo.

“Unayezalisha chupa za rangi au kutumia weka utaratibu wa kuzinunua au kuhamasisha jamii wakuletee kwa gharama zako,” amesema Dk Gwamaka.

Hata hivyo, Dk Gwamaka amesema kuna baadhi ya viwanda vimekuwa na utaratibu wa kuzikusanya chupa hizo na kuweka miundombinu ya kuzirejeleza, akipongeza jitihada hizo zinazolenga kulinda mazingira.

Miaka kadhaa iliyopita aliyewahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba alisema kuzagaa mitaani kwa chupa hizo za rangi kunatokana bei ya wanunuzi kuwa ndogo hali inayosababisha kutowatuvia waokotoaji.

Waziri Makamba alifafanua kuwa bei chupa za rangi ni kati ya Sh80 au 100 kwa kilo. Wakati huo huku chupa nyeupe zinanunuliwa kwa Sh400 kwa kilo.

Katika hatua nyingine, Dk Gwamaka amewataka wachimbaji wakubwa, wa kati na wadogo wa madini, kuhakikisha wanakuwa makini na mabwawa yao ya tope sumu ili kulinda na kuhifadhi mazingara wakati huu, mvua zinaendelea kunyesha.

Dk Gwamaka amesema mvua zikiwa nyingi baadhi ya mabwawa yenye tope sumu yanajaa kupita uwezo wake na kusababisha athari kwa mazingira.

“Huu ni muda mwafaka kwa wote wanaomiliki mabwawa yenye tope sumu, kuyaratibu vyema na kutoa taarifa kwa mamlaka husika pindi wanapoona kuna viashiria vya kupasuka,” amesema Dk Gwakama.

Jana Jumatatu, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ilisema mvua zitaendelea kunyesha kwa siku tano kuanzia jana katika mikoa ya Kagera, Geita, Mara, Katavi, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Manyara, Morogoro, Arusha na Kilimanjaro na Dar es Salaam.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live