Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Katibu Mkuu wa zamani ataka sheria ya ‘blue print’ uchumi

Uchumi Kupanda Katibu Mkuu wa zamani ataka sheria ya ‘blue print’ uchumi

Fri, 6 Oct 2023 Chanzo: mwanachidigital

Katibu Mkuu wa zamani wa Wizara ya Biashara na Viwanda, Uledi Mussa amesema licha ya Tanzania kuwa na sera nzuri ya uchumi ‘blue print,’ lakini haiwezi kutekelezeka kwa kuwa haijatungiwa sheria.

Kauli hiyo ameitoa , Oktoba 05,2023 kwenye mdahalo wa kongamano la kimataifa la viwanda linaloendelea jijini Dar es Salaam, wakati akijibu swali liliulizwa na mwenyekiti wa zamani wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), Dk Samwel Nyantahe aliyehoji na kutaka kujua utekelezaji wa mpango huo kwa kuwa una manufaa.

Katika mdahalo huo uliokuwa ukiongozwa na Balozi John Ulanga ukiwa na mada, 'Nini Changamoto, Fursa na Suluhisho kwenye Sekta ya Uwekezaji na Biashara nchini, katika majibu yake, Mussa alikiri sera hiyo kuna na mambo mazuri ya kuchochea mazingira ya uwekezaji lakini kukosekana kwa sheria kuna weka kigugumizi cha utekelezaji wake

"Blue Print ina mambo mengi mazuri na wakati tunabuni tulisema kwa sababu haya mambo yanagusa maisha ya wengi tena ya wakubwa na ya kitaasisi na binafsi kuna haja ya kuifanya kubwa sheria ipitishwe bungeni hakuna mtu atakayepinga sheria," amesema

Katika maelezo yake amesema wakati mpango huo unaanzishwa alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Uwekezaji, na lengo lilikuwa ni kuishawishi benki ya dunia iitaje nchi ya Tanzania kama moja ya eneo lenye mazingira mazuri ya ufanyaji wa biashara na uwekezaji.

"Msukumo huo tuliupata baada ya benki ya dunia kutoa ripoti ya kila mwaka ikionyesha nchi zinazoongoza kwa mazingira mazuri ya uwekezaji...kila ripoti hiyo ikitoka, Tanzania tuko chini, tulipambana kuweka mpango huo ili tu kuishawishi dunia na hatukutaka kushindana na mataifa mengine," amesema.

Amesema akiwa na wenzake ndani ya wizara hiyo walipambana kutengeneza taratibu na sheria kwa kubainisha zinazopaswa kuwepo, kuboreshwa na zingine kuondolewa kabisa.

"Tulipendekeza taasisi zinazopaswa kuondolewa kwa kuwa kuna utitili wa taasisi za umma zinazosimamia ambazo kila moja inatoza tozo yake ikiwemo Mamlaka ya Udhibiti wa Mafuta, tukiamini Serikali inaweza kuwalipa mishahara hata bila kutegemea kutoza tozo," amesema.

Amesema katika sera hiyo walipendekeza kuondolewa tozo zinazokusanywa na halmashauri, wilaya, mikoa, huku akieleza jitihada hizo zililenga kupunguza urasimu na kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini.

Mchangiaji mwingine kwenye mjadala huo, Falesy Kibassa amesema pamoja na mpango huo bado changamoto ya umeme, barabara na watu kutokusoma kunarudisha nyuma maendeleo ya sekta hiyo.

"Ni muhimu Serikali ikaangalia namna ya kuboresha maeneo hayo hasa eneo la umeme kukatika kwani kunaleta woga kwa wenye mitaji kuja kuwekeza nchini," amesema Kibassa.

Chanzo: mwanachidigital