Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Katibu Mkuu EAC kazitaja faida za Tanzanja na Burundi kusaini mkataba wa AfCFTA

A04e46dab545b6f6c0ca70407d88f40f.jpeg Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)

Tue, 14 Sep 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dk Peter Mathuki, amezipongeza Tanzania na Burundi kwa kuridhia Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) baada ya Burundi kuridhia mkataba huo Juni 17, 2021 huku Bunge la Tanzania likiridhia mkataba huu Septemba 9, mwaka huu.

Nchi nyingine washirika wa EAC zilizoridhia mkataba huo ni Kenya, Rwanda na Uganda huku Jamhuri ya Sudan Kusini imesaini mkataba wa AfCFTA, lakini haijathibitisha. Mathuki alisema AfCFTA itawezesha wananchi wa EAC kupata soko kubwa Afrika na kuongeza mauzo ya nje ya Jumuiya ya Afrika kwa nchi nyingine zilizo nje ya jumuiya.

“Itaboresha pia mwingiliano wa watu Afrika, kukuza biashara na maendeleo na hatimaye kuifanya EAC kuwa katika nafasi nzuri ya kufanya biashara zaidi duniani,” alisema Mathuki. Alisema EAC imeanzisha hatua mbalimbali katika kuelekea utekelezaji wa Mkataba wa AfCFTA na kwamba, kuridhiwa kwa mkataba huo na nchi za Burundi na Tanzania kutaharakisha utekelezaji wa makubaliano hayo.

Dk Mathuki amesema kuwa EAC iko karibu kukamilisha uwasilishaji wa ofa zake za ushuru. “Tumeandaa pia rasimu ya mkakati kwa ajili ya utekelezaji wa mkataba huo, ambao unazingatia hitaji la kuwajengea uwezo wananchi na kwa sasa inafanywa kazi na nchi wanachama,” alisema Dk Mathuki. Katibu Mkuu alisema kuwa ni matarajio ya EAC kwamba, AfCFTA itasaidia pamoja na mambo mengine, kupungua kwa gharama za biashara, kukuza biashara ya ndani na kuwa eneo la utatuzi wa migogoro.

Chanzo: www.habarileo.co.tz