Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Katazo la uvuvi wa kamba laibua sintofahamu Rufiji

20153 Pic+uvuvi TanzaniaWeb

Tue, 2 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hatua ya Serikali kuzuia uvuvi wa samaki aina ya kambamiti (prawns) kuanzia Septemba mwaka huu hadi Machi 2019 na ukataji wa miti ya mikoko kwa ajili ya biashara, imezua sintofahamu kwa wakazi wa vijiji vya Kiomboni, Mchinga, Mfisini, na Nyamisati vyote vikiwa ndani ya Kata ya Salale, Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya utafiti kubaini kupungua samaki hao kwa kasi kutokana na uvuvi uliopitiliza.

Mwandishi wa habari hizi alisafiri kwa mtumbwi kutoka gati ya Nyamisati hadi katika vijiji hivyo vilivyo mithili ya visiwa na kujionea hali ya kusikitisha ya wananchi baada ya kuzuiwa kufanya shughuli hizo hasa uvuvi wanaoutegemea kwa maendeleo ya kiuchumi.

Maelezo ya wananchi

Wakizungumza hivi karibuni kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Mchinga wilayani Kibiti, baadhi ya wananchi wameiomba Serikali kufikiria upya hatua hiyo kwani inahatarisha maisha yao.

Haidari Kipande anayetoka kitongoji cha Saninga, anasema maisha yao yote wamekuwa wakitegemea uvuvi, lakini sasa umewatumbukia nyongo.

Anasema wavuvi wamegawanyika katika makundi matatu ambayo ni wale wanaovua kwa kutumia ndoano, mishipi ya mtego na nyavu za kutanda.

“Kwanza wanaovuliwa ni uduvi, pili chakacha (wote ni dagaa), halafu samaki wa kawaida. Uduvi tangu mababu unajulikana ukubwa wake sawa na ncha ya chelewa ambapo hata watimize miaka 100 watano hawatoshi kwa kitoweo. Chakacha nao ni vivyo hivyo.

“Lakini tunashangaa Serikali inasema tuwaache wakue, tunashangaa. Tangu lini uduvi na chakacha wakakua? Tunahisi huenda tunafanyiwa hiyana ya maisha yetu. Hatuvui samaki, uduvi wala chakacha,” anasema Kipande.

Akizungumzia ukataji mikoko, Kipande anasema miti hiyo ya asili iligawanywa na Serikali na kuwekwa alama.

“Kulikuwa na mashamba ya ‘bibi’ na shamba la wananchi. Maeneo ya wananchi huyatumia kuendesha shughuli zao mbalimbali na maeneo ya Serikali ukiyahitaji inakupasa kupata kibali,” anasema.

Akisimulia zaidi, Kipande anasema mwaka 1931, wazee wao walifyeka mapori ya visiwa hivyo na kushitakiwa na Serikali ya wakoloni, lakini walishinda kesi.

Alisema hata kesi ya kukata miti iliyofanyika mwaka 1957 wakati wa ukoloni katika eneo la Kisanga wanakijiji walishinda.

“Leo maeneo yote ni ya maliasili, imefikia hatua sasa hatujiamini na maisha yetu, tuko karibu na kufa kuliko kuishi. Tunamwomba Rais John Magufuli asikilize kilio chetu”.

Maelezo ya Kipande yanaugwa mkono na Amir Mbonde akisema kitendo cha Serikali kuwazuia kukata miti kwa ajili ya biashara na matumizi mengine ni ukatili na kuwafarakanisha na viongozi.

“Tupo huku kwa muda mrefu tangu mababu. Hata hiyo mikoko wanayotupiga marufuku kuitumia walipanda bibi na babu zetu, waliianzisha mpaka leo inaendelea yenyewe,”anasema na kuongeza:

“Hatupingani na Serikali, kama ni mpango wake kutaka tusitumie rasilimali tulizonazo, lakini basi ituletee kitu mbadala, vinginevyo shule zitafungwa. Au huu ni mpango wa kuhakikisha watu wa Pwani hatupati elimu,” anasema.

Anaendelea kusema: “Kwetu viwanda vya kutoa ajira ni majahazi ambapo kila moja lina watu 10 wanaolihudumia. Kwa mfano kukiwa na majahazi 10 hapo kuna wafanyakazi 100. Endapo kila mmoja atakuwa anategemewa na mtu mmoja tu nyuma yake ina maana kuna watu 200 wanaotegemea majahazi hayo. Kama hii ni Serikali ya viwanda mbona vyetu vinakoseshwa kazi, tutaishi vipi?”.

Kutokana na kuzuiwa kwa shughuli hizo, Tatu Kisukulu anasema maisha yao yamekuwa magumu ikiwemo upatikanaji wa huduma za jamii ambao sasa umekuwa duni.

“Tunasomesha watoto wetu kwenye ngazi tofauti ikiwemo sekondari. Binafsi nina watoto watatu na wajukuu ambao mama zao wamefariki, wote wananitegemea. Mume wangu kazi yake ni uvuvi ambao serikali imetufungia,” anasema.

Naye Hadija Yusufu anaungana na wenzake akisema matumizi ya rasilimali zinazopatikana humo yameingia mkosi.

“Uvuvi hakuna, kukata miti hakuna, hayo ndiyo maisha yetu. Tutaishi vipi bila vitu hivyo? Tunamwomba ndugu yetu, baba yetu Rais Magufuli asikie kilio chetu tunaangamia wananchi wake. Hatujui kama tutafika 2020. Ikimpendeza atoe kauli njema kwetu kuhusu jambo hili tutashukuru,” anasema Hadija.

Kwa upande wake Kesi Moshi anahoji sababu ya kutaifisha majahazi yenye miti na kuyatoza faini bila kuirejesha kijijini hapo.

“Majahazi yetu yanapobeba miti yakifika mbele ya safari yanakamatwa na kupigwa faini. Tunahoji fedha hizo zinakwenda wapi wakati huku vijijini, huduma za matibabu katika zahanati tunachangia, madaftari na kalamu tunanunua, je fedha zinazotoka vijijini mwetu zinakwenda wapi?” Anahoji Moshi.

Akifafanua zaidi, Yusuf Hakungwa maarufu Kolimba anasema mwaka jana, Serikali ilipotangaza kusitisha uvuvi wa kambamiti kuanzia Septemba 1, mpaka Agosti 31, mwaka huu, wananchi walikutana na Naibu Waziri wa Uvuvi na Mifugo, Abdallah Ulega ambaye pia ni Mbunge wa Mkuraga akiwa na Mbunge wa Kibiti, Ally Ungando na kumweleza kero hiyo.

Anasema walizungumzia changamoto hizo kwa kina jinsi gani hatua hiyo ya Serikali inavyowaathiri katika maisha ya kiuchumi.

“Wananchi tulimweleza kutoka Septemba 1, mpaka Machi 31 ni siku za mavuno katika maeneo yetu. Hatupingani na Serikali, lakini tunaiomba, kama ni kufunga ianze Aprili hadi Julai.

“Sababu tulizotoa ni kwamba, wananchi wa maeneo haya ya Delta ya Rufiji kipindi hicho ni cha masika, kwa hiyo bahari yetu inabeba maji baridi na uvuvi wa kambamiti hatupati. Kwa hiyo kipindi hcho ni sawa na mapumziko,” anasema Kolimba.

Anasema baada ya Waziri Ulega kuwasikiliza aliwataka wachague wawakilishi sita ili wakutane Dodoma kwa ajili ya kuwasilisha kero hiyo kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina. Lakini mpaka leo hakuna kilichofanyika.

“Naibu Waziri Ulega alitupeleka kwa Waziri Mpina tukajieleza. Waziri akatwambia nendeni mkakae wiki moja nitawapa ufumbuzi wa tatizo hilo, lakini mpaka leo hatujapata maelezo yoyote,” anasema.

Uongozi wa Wilaya

Licha ya mawaziri kutopatikana kuzungumzia suala hilo, uongozi wa Wilaya ya Kibiti unakiri kupokea barua ya katazo la uvuvi wa kambamiti na umeridhia kutokatwa kwa miti ya mikoko.

Akizungumza na mwandishi wa Mwananchi ofisini kwake, Mkuu wa Wilaya hiyo, Gulam Kifu alisema: “Hili suala la kambamiti tulipewa kabisa maelekezo na Wizara kwamba uvuvi wake usitishwe kuanzia Septemba hadi April. Sasa kama kuna mkanganyiko kwamba wao wanaona wabadilishiwe, basi waombe,” anasema Kifu.

Hata hivyo, anasema hilo siyo tatizo kubwa kwa kuwa wananchi wa wilaya hiyo hawaishi kwa kutegemea samaki hao pekee.

“Tuna samaki wa kila aina, mtu akisema maisha yetu ni kambamiti tu huyo ni mwongo. Zipo maliasili ambazo Serikali inaona kuna umuhimu zilindwe, vinginevyo zitapotea kabisa, na hawakuambiwa wasivue kabisa, hapana kuna wakati wanakatazwa na muda mwingine wanaruhusiwa kuvua,” anasema.

Akifafanua zaidi, Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wilayani humo, Mathew Ntilicha alisema eneo la vijiji hivyo ni la hifadhi, japo vinatambuliwa kisheria.

“Hilo ni suala la kihistoria, lakini wajiulize, wako pale kisheria? Lile ni eneo la hifadhi. Ndiyo maana Septemba 28, mwaka 2016 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea kule alisitisha shughuli zote,” alisema Ntilicha.

Aliongeza: “Ni kweli vile vijiji vinatambulika, lakini sheria ya uhifadhi nayo inawabana. Kwa hiyo wanapoishi wako kihalali ila hawatakiwi kugusa rasilimali zilizopo. Ni sawa na kujenga katika hifadhi ya barabara, ukigongwa na gari utamlaumu nani?”

Hata hivyo, Ntilicha anasema kwa sasa Serikali ina mpango wa kuanzisha utalii wa mazingira na mpango wa usimamizi wa misitu kwa kushirikiana na taasisi ya Wetland International utakaowashirikisha pia wananchi.

“Yale mambo ya zamani ya kukata miti na kupeleka walikokuwa wakiipeleka hayapo tena. Awali tulilala lakini sasa tuko macho,” anasema.

Kambamiti

Akizungumzia zuio la uvuvi wa kambamiti, Ofisa Uvuvi wa wilaya hiyo, Faraja Nyamwombo anasema limefanyika baada ya matokeo ya utafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (Tafiri).

“Upatikanaji wa kambamiti umekuwa ukipungua siku hadi siku. Utafiti ulionyesha kupungua kwa kiwango kikubwa tangu mwaka 1982 hadi 2000. Mwaka 2007, Wizara ilisitisha uvuvi wa kibiashara na kuwaacha wavuvi wadogo,” anasema na kuongeza:

“Hata hivyo, ilionekana kuwa wavuvi wakubwa waliwatumia wavuvi wadogo kuendeleza uvuvi. Tafiri ilifanya utafiti mwingine miaka ya 2009, 2011 na 2014 ikaonekana bado wanapungua kwa kasi. Mwaka 2017 wavuvi wadogo nao walipigwa marufuku.”

Akizungumzia juhudi za wilaya hiyo kuwasaidia wavuvi wadogo, alisema walifanya nao kikao mapema mwaka huu kujadili katazo hilo na njia mbadala za kujikwamua.

“Tulipowauliza kuhusu muda mwafaka wa kusimamisha uvuvi, hata wao kwa wao wanapishana. Wengine wanakubali muda huu wengine wanasema haufai. Hata hivyo, mapendekezo yao yamechukuliwa,” anasema.

Anasema kwa sasa wana mpango wa ujasiriamali kwa wavuvi unaofadhiliwa na Mfuko wa Kimataifa wa Hifadhi za Asili (WWF) ambapo wavuvi wanapaswa kuandika madokezo ili wafadhiliwe.

Kuhusu zuio la uvuvi wa kambamiti, Mbunge wa Kibiti, Ungando anasema tatizo lipo kwenye muda uliowekwa.

“Sisi wananchi tunaona huo muda waliofungia uvuvi ndiyo wa mapato. Wamefungia kuanzia Septemba hadi Aprili, sisi tunataka wafungie kuanzia Jauari hadi Julai,” anasema Ungando.

Akizungumzia juhudi alizozifanya, anasema ameshazungumza na Waziri wa Mifugo na Uvuvi na kujibiwa kwamba tayari kuna wataalamu wameshatumwa vijiji kufanya tathmini.

Chanzo: mwananchi.co.tz