Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Karafuu kununuliwa ‘kielektroniki’

632f587c5f3b3695acd1412c0fd711d7 Karafuu kununuliwa ‘kielektroniki’

Wed, 20 Jul 2022 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Shirika la Taifa la biashara (ZSTC) limeanza kununua karafuu kutoka kwa wakulima katika msimu mdogo wa mavuno huku likisitiza kutumia mashine za kielektroniki za kuchambua uchafu.

Lengo la mashine hizo ni kuona ubora wa karafuu zinazonunuliwa kutoka kwa wakulima unaimarika.

Hayo yalisemwa na Ofisa Elimu Mwandamizi wa ZSTC, Abdalla Ali wakati akiwakaribisha wakulima kuuza karafuu zao katika kituo cha Piki, Mkoa wa Kaskazini Pemba kuashiria kufungua msimu wa mavuno ya karafuu.

Alifahamisha kuwa shirika limejipanga kuhakikisha linanunua karafuu kutoka kwa wakulima zikiwa na ubora unaohitajika kwa ajili ya kuingia katika soko la kimataifa.

Alisema katika hatua hiyo, shirika hilo limeamua kununua mashine mpya za kielektroniki za kuchambua uchafu baada ya kupata hasara ya Sh bilioni tatu msimu uliopita.

Awali, Ofisa Biashara wa shirika hilo, Twahiri Ali Saleh alisema mashine hizo zinagawiwa katika vituo muhimu vya kununua karafuu kwa lengo la kuhakikisha karafuu inayonunuliwa mwaka huu na inakuwa na ubora unaotakiwa.

Alisema hapo nyuma kulikuwa kumejitokeza baadhi ya wakulima kufanya hadaa kwa kuchanganya karafuu na vitu mbalimbali ikiwemo takataka na makonyo na kuleta shida katika soko la karafuu la kimataifa.

Saleh alisema biashara ya karafuu imekuwa na ushindani mkubwa katika soko la kimataifa ingawa karafuu ya Zanzibar ndio imekuwa yenye kupendwa zaidi kutokana na ubora wake.

Baadhi ya wakulima waliouza karafuu zao katika kituo cha Piki, Wilaya ya Wete walieleza kufurahishwa na matumizi ya mashine hizo ambazo zitawawezesha wakulima kuchukua tahadhari zaidi ya usafi wa karafuu zao wanazouza.

''Mimi sina wasiwasi na matumizi ya mashine hizi ambazo zipo kwa ajili ya kupima ubora na kuchambua uchafu uliomo katika karafuu zinazouzwa katika vituo vya ZSTC,'' alisema Hamadi Bakari ambaye aliuza gunia tatu za karafuu.

Chanzo: www.habarileo.co.tz