Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kanuni 3 kusimamia biashara ya tanzanite

Bd834596dbf479018e95a5b0b8bd461d Kanuni 3 kusimamia biashara ya tanzanite

Mon, 19 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI imepitisha marekebisho matatu ya kanuni za biashara ya madini ya tanzanite kwenye mgodi wa Mirerani, wilayani Simanjiro, mkoa wa Manyara.

Mabadiliko hayo madogo kwenye Kanuni za Uendeshaji wa Eneo Tengefu la Mererani yalipitishwa rasmi Julai 9, mwaka huu na utekelezaji wake ulianza siku hiyo hiyo.

Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila alisema hayo wakati akizungumza na HabariLEO jana.

Alisema kurekebishwa kwa kanuni hizo ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilolitoa Julai 7, mwaka huu wakati akizindua kituo cha tanzanite cha Magufuli, Mirerani

Kwa mujibu wa Profesa Msanjila, kupitia mabadiliko hayo ya kanuni, serikali imeweka zuio kwamba kuanzia sasa, biashara ya madini ya Tanzanite itafanyika Mirerani tu na si mahali pengine popote.

Alisema kabla ya mabadiliko hayo, biashara ya madini hayo ilikuwa inaweza kufanyika katika soko lolote.

“Awali ilikuwa kwamba mtu akipata madini ya tanzanite kutoka kwenye ukuta wa Mererani alikuwa anaweza kuamua kwa mfano madini hayo anataka kwenda kuyauza kwenye soko la Dar es Salaam, hivyo anapewa kibali cha kusafiri nayo kwenda soko la Dar es Salaam, na Dar es Salaam wanakuwa wameshajua kwamnba kuna mzigo wa tanzanite unatoka Mirerani kwa sababu kuna mfumo tayari,” alisema Profesa Msanjila na kuongeza:

“Lakini kwa sasa kutokana na mabadiliko haya ya kanuni, hataruhusiwa, atauza tanzanite yake Mirerani, yakishakatwa na kuwa bidhaa kama vile pete au bidhaa nyingine yoyote, hiyo sasa inaweza ikatoka eneo nje ya Mirerani na kwenda kuuzwa popote kwa kuwa imekuwa bidhaa na si madini.”

Marekebisho ya pili ya kanuni hiyo yameweka zuio kwamba, leseni za wafanyabiashara wakubwa wa madini uhalali wake wa kushughulika na tanzanite utakuwa Mirerani tu.

Profesa Msanjila alisema mfanyabiashara huyo anaweza kuitumia leseni yake sehemu nyingine kununua madini ya aina nyingine lakini si kwa tanzanite.

Alisema marekebisho hayo yanamtaka mfanyabiashra kama anataka kushughulika na tanzanite lazima awe Mirerani ndani ya ukuta au eneo lingine lililotengwa na Tume ya Madini ndani ya Mirerani.

“Marekebisho ya tatu ni kwamba kanuni inataka ukataji madini ya Tanzanite ufanyike Mererani tu. Kwa sababu Waziri Mkuu aliagiza kwamba ndani ya siku 90 tangu kutoka kwa tangazo lile au mabadiliko yale ya kanuni, ukataji ufanyike Mirerani tu. Kwa haya ndiyo mambo matatu yaliyoongezwa kwenye Kanuni za Uendeshaji wa Eneo Tengefu la Mererani,” alisema Profesa Msanjila.

Kuhusu agizo la Waziri Mkuu la kuwataka wafanyabiashara ya madini wa tanzanite wote kuhamia Mererani ndani ya miezi mitatu, Profesa Msanjila alisema tayari wafanyabiashara hao wameshaanza kuhamia katika eneo hilo.

Alisema kwa sasa manunuzi ya tanzanite yanafanyika Mirerani na miezi mitatu ilitolewa kwa wafanyabiashara wa madini hayo kuhamishia viwanda vyao vya ukataji wa madini hayo eneo hilo na tayari wameanza kutekeleza agizo hilo.

Profesa Msanjila alisema kama shughuli za manunuzi ya tanzanite zingekuwa hazijahamia Mirereani, wachimbaji wadogo wangeshapiga kelele kwa kuwa kazi yao ni kuchimba na kuuza kila siku.

Chanzo: www.habarileo.co.tz