Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kanda ya Kaskazini inavyobeba utalii Tanzania

Utalii Kinara Kenya Kanda ya Kaskazini inavyobeba utalii Tanzania

Tue, 9 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Asilimia 58.7 ya mapato yote ya utalii yaliyopatikana katika mbuga za wanyama mwaka 2022/2023, yalitokana na vivutio vinavyopatikana Kanda ya Kaskazini, Ripoti ya Benki Kuu Tanzania (BoT) imeeleza.

Ripoti hiyo ya Uchumi ya Kikanda 2022/2023 inaonyesha, kuongoza kwa kanda hiyo katika mapato ya utalii kunatokana na idadi kubwa ya watalii kuchagua eneo hilo kama sehemu yao ya kupumzikia.

Uchambuzi unaonyesha, zaidi ya Sh463.34 bilioni zilipatikana kupitia watu mbalimbali kutembelea mbuga za wanyama mwaka 2022/2023 ikiwa ni ongezeko la asilimia 43.4 ikilinganishwa na Sh323.2 bilioni zilizopatikana kipindi kama hicho mwaka uliotangulia.

Fedha hizo zilipatikana kupitia watembeleaji, milioni 2.2 waliotembelea mbuga za wanyama katika mwaka huo wa fedha ikilinganishwa na watembeleaji milioni 1.8 waliokuwapo mwaka uliotangulia.

Kati ya watalii hao, Kanda ya Kaskazini pekee ilipokea watalii milioni 1.43 ambayo ni sawa na asilimia 65.4 ya watalii wote nchini huku ikijiingizia Sh271.98 bilioni.

Akizungumzia suala hilo, Mtaalamu wa Uchumi, Profesa Aurelia Kamuzora amesema maliasili zilizopo kaskazini ndiyo zinafanya watu wengi kuchagua eneo hilo kama sehemu yao kutalii kutokana na upekee wake.

“Kanda hii kuna sehemu zinavutia, ukienda Kilimanjaro, ukienda Ngorongoro, kuna maporomoko ya maji chemka hivi ni vitu huwezi kupeleka sehemu yoyote, ni suala na asili lililopo, ila tuendelee kutangaza vivutio vingi ambavyo havijajulikana.

Amesema yapo maeneo ambayo yanaweza kutumika vizuri na kuingiza fedha nyingi za kigeni kama yatatangazwa vilivyo kama hifadhi ya maua ya Kitulo, Kimondo kilichopo Mbeya, chemichemi zilizopo nchini tofauti na kanda ya Kaskazini.

Kanda nyingine

Kanda ya Ziwa ilifuata kwa kuingiza asilimia 36.6 ya mapato hayo ambayo ni Sh169.39 bilioni kupitia watalii 525,497 iliohudumia katika mwaka wa fedha 2022/2023.

Kusini Mashariki iliingiza Sh12.66 bilioni kupitia watalii 86,722 iliyowahudumia ikiwa ni ongezeko la watalii la asilimia 45.7 ikilinganishwa na waliokuwapo mwaka uliotangulia.

Kanda ya kati ilishika namba tatu kwa kuingiza Sh5.08 bilioni kupitia watalii 115,443 iliyopokea katika mwaka huo wa fedha ikiwa ni ongezeko la watalii kwa asilimia 54 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.

Nyanda za juu kusini Sh4.2 bilioni ziliingizwa kupitia watalii 44,175.

“Tutumie Kaskazini kuvuta watalii waende sehemu nyingine zilizopo nchini, hiyo sehemu iwe kama geti kufika maeneo mengine kwa sababu hatuwezi kuhamisha vivutio kwenda maeneo mengine,” amesema Profesa Kamuzora.

Makumbusho ya Taifa

Katika upande wa makumbusho ya taifa yaliyopo nchini, mapato yake yaliongezeka kwa asilimia 6.3 hadi kufikia Sh78.94 bilioni mwaka 2022/2023.

Dar es Salaam iliongoza kwa kubeba asilimia 79.5 ya mapato yote yaliyopatikana katika mwaka huo ambayo ni Sh72.6 bilioni huku ikibeba asilimia 63 ya watembeleaji wote.

Hata hivyo, watembeleaji 49,776 waliokuwapo katika mwaka huo, ni pungufu ya asilimia 8.7 ya wale waliokuwapo mwaka uliotangulia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live