Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kampuni zinazohitaji malighafi ya plastiki zaongezeka

Mon, 3 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc), Dk Samuel Gwamaka amesema kuna kampuni tano zimeonyesha nia ya kuichukua mifuko ya plastiki iliyokusanywa kwa ajili ya kuzalisha vyombo vya nyumbani ikiwamo ndoo za plastiki.

Pia, Dk Gwamaka amesema mbali ya kampuni hizo, kuna viwanda vinne vya saruji vimejitokeza kuitaka mifuko hiyo kwa ajili matumizi ya chanzo cha nishati katika uzalishaji wake.

Ametoa kauli leo Jumamosi Juni mosi katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Zakhem Mbagala uliohudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyniva.

Dk Gwamaka amesema wanaendelea na mazungumza na viwanda na kampuni kuhusu uchukuaji mifuko hiyo itakayotumika kama malighafi ya bidhaa mbalimbali na chanzo cha nishati.

"Mifuko ya plastiki itakayokusanywa itakuwa ya aina mbili, itakayokuwa misafi na michafu. Tutaichambua ile misafi itapelekwa huko," amesema Dk Gwamaka.

Mbali na kampuni na viwanda hivyo, hivi karibu  Makamba alisema kuna kampuni nyingine tatu ikiwamo ya Falcon ya Mwanza zimejitokeza kuhitaji mifuko ya plastiki kwa ajili ya kuzalisha mabomba ya maji na madawati.

Pia Soma

Katika hatua nyingine, mmoja wa wajasiriamali wa kuzalisha mifuko mbadala ya karatasi, Jonesia Sebastian amewahakikisha Watanzania mifuko maalumu ya   kubebea bidhaa kama nyama na utumbo imeshatengenezwa na kusambaza kwenye maeneo mbalimbali.

"Niwatoe hofu mifuko hii ipo na ni tofauti na ile ya kuhifadhia nyaraka mbalimbali, watu wasiwe na wasiwasi kuhusu bidhaa kama nyama na utumbo. Bei ya mifuko itaanza Sh100 kwa mfuko mmoja wa kilo moja na kuendelea.

"Mifuko hii ni migumu na ukiweka nyama inakaa zaidi saa mbili bila mfuko kutoboka wala kuloa," amesema Sebastian huku akipigiwa makofi na wakazi waliohudhuria mkutano huo.

Chanzo: mwananchi.co.tz