Katavi. Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Japhet Hasunga amesema kampuni zinazoagiza mbolea nje ya nchi, miaka mitatu ijayo hazitapewa vibali kama hazitajenga viwanda vya kutengeneza au kuchanganya mbolea nchini.
Pia, amewataka wawekezaji na taasisi mbalimbali kuzalisha mbolea nchini ili kusaidia bidhaa hiyo kushuka bei kwa kuwa ikiagizwa nje bei yake huwa juu.
Ametoa agizo hilo jana Jumapili Oktoba 13, 2019 mjini Mpanda katika maadhimisho ya siku ya mbolea duniani ambayo kitaifa imefanyika mkoani Katavi.
"Hatuwezi kuendelea kuagiza mbolea kutoka nje wakati mwaka 2025 tunataka kufikia Tanzania ya viwanda.”
“Lazima tufike asilimia 50 ya kuzalisha mbolea yetu vijana wetu watapata ajira, mbolea tutatengeneza inayoendana na udongo na bei itapungua," amesema Hasunga.
Amewataka wafanyabiashara wa mbolea kuzisambaza mikoani kutokana na msimu wa kilimo kuanza.
Pia Soma
- Maaskofu Katoliki Tanzania kuratibu mchakato wa kumtangaza Mwalimu Nyerere Mtakatifu
- CUF yatoa sababu wananchi kutojitokeza kujiandikisha kupiga kura
- VIDEO: Mhagama: Miradi 107 ya maendeleo ina kasoro
"Sio mkurugenzi mkuu mnawapa watu tenda hawana maeneo, sasa huyu mnayempa ambaye hana wakala, ghala hata sehemu ya kupeleka, anafanyia biashara Dar es Salaam, hatutaki mafisadi wa namna hiyo, kila mfanyabiashara awe na mtandao utakaosaidia kusafirisha mbolea nchi nzima," amesema Hasunga.
Ameongeza, "kama hapa Katavi hakuna sababu ya msingi kusafirisha mbolea kwa magari, kwa nini tusisafirishe kwa treni ambayo ikishusha magari ndio yapakie na kupeleka vijijini ili kupunguza gharama.”
"Naiagiza mamlaka ya kudhibiti mbolea Tanzania TFRA kuhakikisha wanazingatia ubora. Mbolea ikaguliwe inapoingia bandarini, inavyofungashwa, inavyosambazwa na kusafirishwa, kila mfanyabiashara azingatie sheria,"
Naye mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera amesema Mkoa huo una changamoto ya upungufu wa maofisa ugani unaosababisha wakulima kukosa elimu ya kilimo cha kisasa.
"Tutafutiwe wataalamu wa kilimo watoe mafunzo kwa maofisa watendaji wa vijiji na kata ili wasaidie kutoa elimu kwenye maeneo yao. Uwezo wa kuajiri kila kijiji hakuna iwe sawa na mfungwa hachagui gereza, hii itasaidia sana," amesema Homera.
Richard Hamu, mkulima wa tumbaku na mahindi mkoani Katavi amesema changamoto iliyowakabili kwa muda mrefu ni ucheleweshwaji wa pembejeo za kilimo.