Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kampuni zapewa siku 21 kuwasilisha taarifa BRELA

Brela Mkl.jpeg Kampuni zapewa siku 21 kuwasilisha taarifa BRELA

Tue, 14 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni nchini (BRELA), imewataka wamiliki wa kampuni, kuwasilisha taarifa zao za umiliki, ndani ya siku 21, zifanyiwe kazi ya utambuzi na msajili kwa mujibu wa sheria ili wafanye kazi zao kwa uhuru kabla ya kuchukuliwa hatua.

Maelekezo hayo yalitolewa juzi na Kaimu Mkuu wa sehemu ya kampuni kutoka BRELA, Leticia Zavu, wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wamiliki wa kampuni, wanasheria na washauri wa biashara mkoani hapo namna ya kutambua umuhimu wa kusajili shughuli zao.

Zavu, aliwaeleza washiriki hao umuhimu wa dhana ya wamiliki manufaa katika kuhuwisha taarifa za kampuni ili kupata zote za waliokwisha kujisajili BRELA na kujua wanufaika halisi wa hisa zinaonekana kwenye daftari la msajili wa kampuni kutambua mnufaika halisi wa hisa hizo.

Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili, Kanda ya Mbeya, Alfredy Chapa, alisema serikali imeboresha sheria ya kampuni ili kudhibiti baadhi ya mambo ikiwamo utakatishaji wa fedha na vitendo vingine vya rushwa.

“BRELA kwa kushirikiana na wataalamu Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, iliunda kanuni ya kudhibiti mianya ya rushwa, vitendo vya ugaidi utakatishaji wa fedha kwa kampuni zote zilizosajiliwa,” alisema Chapa.

Ofisa Biashara Mkoa wa Mbeya, Stanley Kibakaya, aliiomba BRELA kuweka taarifa zake kwa lugha ya Kiswahili ili iwe rahisi kwa wamiliki wa kampuni kujaza taarifa zote zinazohitajika wakati wa usajili.

Alisema kwa kufanya hivyo kutaongeza mwamko wa wamiliki kutoka maeneo mbalimbali nchini kujitokeza kujaza taarifa zao kwa sababu lugha itakayotumika ni ya Kiswahili.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo akiwamo Kassim Mpika, alisema mafunzo hayo yamekuwa na tija kwao kwa kuwa wametambua utaratibu unaotakiwa kuzingatiwa ili kumiliki hisa kupitia kampuni zao.

Naye Wakili wa kujitegemea mkoani Mbeya, Salome Mwakalonge, alisema umuhimu wa kujaza taarifa za umiliki wa kampuni kupitia BRELA una lengo la kudhibiti mianya ya rushwa na kuongeza pato kwa serikali ili fedha zinazopatikana zitumike kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

Hata hivyo, katika kusogeza huduma za usajili wa kampuni, biashara na leseni, BRELA, imekasimu madaraka kwa maofisa biashara wa mikoa kusimamia zoezi hilo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live