Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kampuni za simu zatakiwa kupanua huduma

B136786c36502d1b1042c29d175399cc Kampuni za simu zatakiwa kupanua huduma

Thu, 11 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WIZARA ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, imezitaka kampuni zinazohusika na mitandao ya mawasiliano ya simu, kupanua wigo wa uwekezaji ili kuhakikisha huduma zake zinapatikana maeneo yote katika nchi nzima.

Kampuni hizo zimetakiwa kupanua uwezo wake wa kusimika minara ya mawasiliano katika maeneo ambayo yanapata changamoto ya mawasiliano ili kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo, wanapata mawasiliano hayo.

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Kundo Mathew alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Grace Tendega (Chadema).

Tendega alisema wananchi wa Kalenga Mkoa wa Iringa, wamekuwa wakipata mawasiliano yasiyo mazuri kwa kuhangaika kutafuta mawasiliano. Alihoji ni lini serikali itahakikisha mawasiliano yanakuwa bora katika vijiji vya Kalenga.

Mathew alisema serikali ina imani kwamba nchi itakuwa na mawasiliano bora kutokana na mitandao ya mawasiliano imara na itahakikisha azma hiyo inatimia.

“Serikali imeziagiza kampuni zinazotoa huduma za mawasiliano kuhakikisha zinaboresha uwezo wa kusambaza mawasiliano katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha wanapata mawasiliano kwa uhakika katika nchi nzima,” alisema.

Akijibu swali la msingi la Mbunge wa Mbulu Vijijini, Flatey Massay (CCM) aliyetaka kujua Kata za Endahagichen – Ndamilay, Mewadan – Magong na Endaghadat – Qamtananat ambazo hazina mawasiliano ya simu, lini minara ya simu itajengwa katika kata hizo, Mathew alisema serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote(UCSAF) na wadau wengine wa sekta ya mawasiliano, ina jukumu la kufikisha huduma za mawasiliano maeneo yote ya vijijini na mijini yasiyo na mvuto wa kibiashara.

“Hadi sasa jumla ya kata 633 zimeshapata huduma za mawasiliano nchi nzima ambapo ujenzi unaendelea katika kata zingine 361 kupitia ruzuku ya serikali,”alisema.

Alisema watoa huduma kwa uwekezaji wao, wamefikisha huduma za mawasiliano katika kata 1692.

Aidha, Januari 25, 2021 walitiliana saini ya mikataba ya kufikisha huduma za mawasiliano katika kata 59 zenye vijiji 166 katika zabuni ya awamu ya tano.

“Vilevile mwezi huu tutatangaza zabuni nyingine ya awamu ya sita ya kufikisha huduma za mawasiliano katika kata 74 zenye vijiji 206,”alisema.

Mathew alisema UCSAF ina miradi 15 Jimbo la Mbulu Vijijini katika kata 13.

Kata zenye miradi ya kufikisha huduma za mawasiliano ni Yaeda Ampa, Yaeda Chini, Maghang, Masieda, Bashay, Eshkesh,Geterer, Gidihim, Hayderer, Maretadu, Masqaroda, Endamilay, na Tumati.

“Jumla ya minara 14 imekamilika kujengwa katika kata 12 kati ya minara 15 inayopaswa kujengwa, hii ni sawa na asilimia 87.5 ya miradi yote katika Jimbo la Mbulu Vijijini,”alisema.

Ujenzi wa mnara uliopo katika Kata ya Endamilay haujakamilika, ambapo Shirika la Mawasiliano Tanzania(TTCL) limepanga kukamilisha ujenzi wa mnara huo kabla ya mwisho wa Juni 2021.

Pamoja na jitihada hizo za serikali, bado kuna kata 1,365 kati ya kata 3,956 zilizopo Tanzania Bara zikiwemo kata za Jimbo la Mbulu Vijijini, na wadi 16 kati ya wadi 111 zilizopo Zanzibar, zina changamoto za upatikanaji wa huduma za mawasiliano.

Alisema serikali kupitia UCSAF inavifanyia tathmini vijiji vya kata za Endahagichen – Ndamilay, Mewadan – Magong na Endaghadat – Qamtananat na vijiji husika vitaingizwa katika orodha ya vijiji vitakavyojumuishwa katika zabuni, zinazotarajiwa kutangazwa katika mwaka huu wa fedha wa 2020/2021.

Chanzo: habarileo.co.tz