Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kampuni za simu zapewa changamoto riba, muda marejesho

Bdd3b87807ade6877ab506bfe4b74421 Kampuni za simu zapewa changamoto riba, muda marejesho

Tue, 18 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAZIRI katika Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Uwekezaji, Angellah Kairuki, amezihakikishia kampuni za simu nchini kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili waweze kuzalisha zaidi kujenga uchumi wa nchi, wao na ajira kwa Watanzania.

Aidha, amezitaka kampuni zisaidie wawekezaji wadogo wazawa kuongeza uwekezaji wao kwa kuwajengea uwezo, kuongeza muda wa marejesho ya mikopo, kupunguza riba na amewataka kuongeza zaidi kiwango cha fedha wanazorejesha kwa jamii kama faida.

Kairuki aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipofanya ziara kutembelea kampuni za simu za mikononi za Vodacom, Airtel, Tigo na Zantel.

Katika ziara hiyo alifuatana na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dk Maduhu Kazi na mwakilishi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya Mawasiliano), Philemon Machaine.

Waziri Kairuki alisema Serikali inatambua pamoja na kufanikiwa kufuta tozo zaidi ya 168 zinazogusa sekta mbalimbali ikiwemo uwekezaji, bado kuna changamoto katika sekta ya mawasiliano zinazochangia kuongezeka kwa gharama za watumiaji wa simu za mikononi.

Kairuki alisema Serikali itaendelea kuzifanyia kazi changamoto hizo ikiwemo kuboresha kanuni na sheria za uwekezaji na kwa kushirikiana na Wizara nyingine ikiwemo ya mawasiliano, na taasisi ikiwemo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na TIC.

Kairuki alizipongeza kampuni hizo kwa namna zinavyochangia kodi kwa Serikali na kuwataka wapunguze muda wa marejesho ya mikopo ya simu na riba kuwa na bei himilivu ili Watanzania wa chini na wa kati wanufaike zaidi.

Mkurugenzi Mkuu wa TIC, Dk Kazi, alisema kituo hicho kitaendelea kufanya kazi kwa karibu na wawekezaji nchini ili kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.

Mwakilishi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Philemon Machaine, alisema Wizara imekuwa karibu kushughulikia changamoto za kampuni za simu nchini na kuziomba ikiwa zinakumbana na vikwazo, wapeleke mapendekezo wizarani.

Chanzo: habarileo.co.tz