Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kampuni za mafuta, gesi zatakiwa kuimarisha mifumo

Gaz System Kampuni za mafuta, gesi zatakiwa kuimarisha mifumo

Mon, 29 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MKUU wa Wilaya ya Kigamboni, Sarah Msafiri, amezitaka kampuni zinazojishughulisha na biashara ya mafuta na gesi zilizomo wilayani humo, kuimarisha mifumo ya kulinda afya na usalama wa wafanyakazi ili kuepuka athari zinazoweza kutokea.

Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akifungua kikao cha mashauriano baina ya wadau wa sekta ya mafuta na gesi pamoja na menejimenti ya Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kilichofanyika katika ofisi ya mkuu huyo Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

“Tunaweza kukwepa vyote, lakini hatuwezi kukwepa suala la usalama kwenye uendeshaji wa shughuli hizi, kwa bahati mbaya sana usalama huu hauwezi kusema wewe unajilinda kwa asilimia mia moja, kama wenzako waliokuzunguka hawana mifumo ya kujikinga kwa kiwango hicho, itakuwa ni kazi bure,” alisema Msafiri.

Aidha, aliwataka wawakilishi wa kampuni za mafuta na gesi waliohudhuria kikao hicho kuwashauri viongozi wao wa juu katika kampuni wanazotoka kuwekeza katika masuala ya usalama na afya ili kuwalinda wafanyakazi pamoja na mali kwa ujumla.

Alisema uwekezaji katika usalama na afya una faida nyingi ikiwamo kuongeza morali miongoni mwa wafanyakazi, kuongeza ubora wa bidhaa na huduma na hivyo kuleta tija katika uzalishaji kwa manufaa ya wawekezaji na serikali kupitia mapato ya kodi.

Baadhi ya washiriki wa kikao hicho akiwamo, Leah John kutoka Kampuni ya Tipper na Moses Mgeni wa kampuni ya MOGAS, waliishukuru serikali kupitia OSHA kwa kuandaa kikao hicho.

Walieleza kuwa imekuwa ni fursa muhimu kwa pande zote mbili (OSHA na wadau) kujadiliana masuala ya msingi ambayo yatasaidia kuboresha mifumo ya usalama na afya katika sekta ya mafuta na gesi ambayo shughuli zake ni hatarishi zaidi kiusalama na afya.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live