Ingawa kampuni za madini zimekuwa na mchango mkubwa kwenye jamii kutokana na kufanikisha miradi ya aina tofauti, wadau wanaona ni wakati muafaka sasa zikjielekeza kuwajengea uwezo wajasiriamali kushiriki kwenye miradi mikubwa yenye manufaa zaidi kwa wananchi.
Maoni hayo yanatokana na ukweli kwamba maendeleo endelevu ya Taifa lolote yatapatikana kwa wananchi kutekeleza miradi ya kiuchumi itakayoboresha kipato cha familia hivyo kuondoa umasikini.
Hata hivyo, sera na sheria za madini, na mafuta na gesi zinahimiza ushirikishaji wa wananchi katika kubuni, kutekeleza na kuendeleza miradi ya jamii katika maeneo inakotekelezwa.
Wakitoa maoni yao kwenye mkutano wa nane wa wadau wa kujitoa kwa kampuni kusaidia miradi ya kijamii (CSR) uliojadili ushiriki wa wanawake katika sekta ya madini, mafuta na gesi jijini Dar es Salaam, waliitaka Serikali na wawekezaji kuangalia upya vipaumbele vya miradi hiyo.
Kwa sasa, kampuni nyingi zinazosaidia jamii huelekeza nguvu nyingi kwenye miradi inayohusu maji, elimu, afya na utunzaji mazingira.
Akizungumza katika mkutano huo ulioandaliwa na Hakirasilimali kwa kushirikiana na ubalozi wa Canada nchini, kiongozi wa miradi ya maendeleo ya kiuchumi ubalozini hapo, Nathalie Garon anasema maendeleo ya wajasiriamali wadogo ni muhimu kuinufaisha jamii nzima
Pia Soma
- Jinsi vyuo vikuu vilivyojipanga kuandaa wataalamu wa viwandani
- Watalii 340 kutoka China ni kama tone la maji baharini
- Baada ya wiki ya mlipakodi, tathmini ifanyike kupima mchango wake
Katika utekelezaji wa miradi hiyo, anasema Canada inasaidia vyuo vya ufundi kutoa mafunzo yatakayosaidia wanafunzi kujiajiri na kuajiriwa katika sekta mbalimbali.
Anasema CSR isiishie kupeleka maji, kujenga shule na kutoa misaada midogomidogo bali iimarishe uelewa wa wananchi namna ya kukuza kipato chao katika mfumo ambao ni endelevu.
“Kipaumbele kitolewe kwa wasichana na wanawake ambao licha ya fursa chache walizonazo, ni wawajibikaji na wanaweza kusimamia vizuri uzalishaji wa huduma na bidhaa,” anasema.
Ofisa wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Esther Mbaga anasema hata Serikali za Mitaa pia zinapaswa kujengewa uwezo ili nazo zishirikiane na wananchi kubuni na kusimamia miradi ya maendeleo itakayoikomboa jamii.
“Sheria zinazipa mamlaka Serikali za Mitaa kujadiliana na kukubaliana na wawekezaji kuhusu utekelezaji wa miradi ya kijamii,” anasema.
Hata hivyo, baadhi ya kampuni zinasema zina programu za kuwawezesha wananchi kielimu. Msemaji wa kampuni ya Total Tanzania, Marsha Msuya anasema wanayo miradi ya mafunzo kwa wahitimu wa vyuo vikuu kabla ya kuwaajiri kwenye kampuni tanzu nje za nchi ikiwamo Malawi, Uganda, Kenya, Uswisi, Afrika Kusini na Nigeria.
“Huwa tunawafundisha namna ya kufanyakazi na kampuni yetu na kuwaajiri hivyo kuboresha kipato chao. Changamoto inayotukabili ni washindani wetu kuwachukua vijana hawa baada ya kuiva kiutendaji,” anasema Marsha.
Mwakilishi wa kampuni ya Cuso International kwenye mkutano huo, Romatus Mtung’e anasema changamoto ya upatikanaji wa mtaji inapaswa kupatiwa ufumbuzi kuwawezesha wananchi kuanzisha miradi ya kiuchumi.
“Sisi tumeanzisha vituo vya uendelezaji wajasiriamali mkoani Mtwara, Iringa na Mwanza. Kampuni nyingine zikiunga mkono vituo hivi, itasaidia kukuza mtaji wa makundi haya,” anasema.
Hata hivyo, naibu mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Maurel and Prom, Elias Kilembe anakosoa dhana ya kuwawezesha wananchi kielimu akisema imewaacha wataalamu wengi wa sekta ya gesi bila ajira.
“Watu wengi walisoma kozi mafuta na gesi wakitumaini kushiriki katika uendelezaji wa rasilimali hiyo baada ya ugunduzi uliofanyika. Lakini, ndoto hizo zimeyeyuka baada ya shughuli hizo kusimamishwa,” anasema.
Mhadhiri mwandamizi wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Dk John Msumba anaamini hakuna uwekezaji unaoweza kuwa na tija kwa wananchi kama si kuwaongezea maarifa.
“Umaskini utaondolewa kwa elimu ili wananchi walime na kufanya biashara kwa tija,” anasema msomi huyo.
Dk Msumba anasema licha ya kuwaunganisha watu katika vikundi kama vile Vicoba, uwekezaji uelekezwe pia katika kuwajengea uwezo wa kufanya mchanganuo wa biashara, namna ya kuchagua biashara bora na mbinu za kupata masoko.
Akizungumza na gazeti hili, mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula aliunga mkono maoni ya wadau hao na kusema tayari amemshauri Waziri wa Madini, Doto Biteko kuangalia namna ya kukabili umasini kwa kuzishirikisha kampuni zilizopo.
Kwa upande wake, Waziri Biteko amesema ofisi yake inawasiliana na Tamisemi kuona namna ambavyo suala hilo litatekelezwa na kwamba haoni tatizo endapo kampuni za madini zitakubaliana na Tamisemi kusaidia kukabili umasikini wa kipato unaowakabili wananchi.