Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kampuni za kati zinahitaji ubunifu ili zidumu sokoni

22418 Pic+ubunifu TanzaniaWeb

Tue, 16 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ili kukuza mapato ya wajasiriamali na mchango wa kampuni za kati kwenye uchumi wa Taifa, mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Biashara la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EABC), Felix Mosha anasema kampuni zinapaswa kuendeleza ubunifu katika nyanja tofauti.

Anasema ni ubunifu pekee ndio utakaoiwezesha kampuni kukabiliana na mabadiliko ya mahitaji ya soko yanayojitokeza kila kukicha yakichangiwa na maendeleo ya teknolojia. “Sasa ulimwengu unatoa kipaumbele katika ubunifu kwani ndio unaokuza kampuni na kuifanya kuwa ya kishindani sokoni. Kampuni inaposhiriki katika shindano hilo hupata fursa ya kujitangaza na kupima utendaji wake kwa kujilinganisha na wengine waliopo katika sekta,” anasema Mosha.

Mosha alikuwa mgeni rasmi wa mashindano hayo kwenye fainali zilizofanyika mwaka 2015 na alizishauri kampuni kufanya kazi kwa ushirikiano ili kupata mafanikio zaidi huku akisema utengano ndio unaoua biashara nyingi nchini.

Takwimu zinaonyesha zaidi ya asilimia 80 ya biashara zinazoanzishwa Tanzania hupotea ndani ya miaka mitano ya kwanza huku sababu kubwa ikiwa ni usimamizi wa familia ambao hauruhusu mawazo kutoka nje kuboresha mfumo wa uendeshaji uliopo. Hata hivyo, Mosha ambaye amekuwa akifuatilia shindano tangu kuanzishwa kwake mwaka 2011 anapongeza kuongezeka kwa programu sanjari na washiriki kila mwaka.

Anasema hiyo ni fursa kwa kampuni za kati kukua zaidi na kutanua mtandao wa wadau waliopo katika jumuiya za wafanyabiashara ndani hata nje ya nchi. Fursa zilizomo kwenye programu za shindano hilo ni muhimu kwani husaidia kuwajengea washiriki uwezo wa kuendesha biashara kwa uwazi na kutambulika zaidi kupitia matangazo mbalimbali yanayoambatana nayo.

Anawapongeza waandaaji na kubainisha kuwa tangu kuanza kwake hajawahi kusikia malalamiko yoyote ya upangaji wa mshindi jambo linalidhihirisha wanatenda haki.

“Jambo kubwa katika mashindano kama haya ni kuhakikisha hakuna upendeleo wala upangaji wa washindi na majaji wanatenda haki kulingana na utaratibu na vigezo vya kuwapata washindi,” anasema Mosha. Kwa vigezo hivyo, anasema faida za shindano hilo ambazo ni kuunga mkono ujasiriamali wa kisasa zitaonekana kwa huwajenga wamiliki wa kampuni kufikiri uendeshaji wa kisasa zaidi.

Mvuto wa Top 100 na utaratibu rahisi wa kushiriki anasema huwachochea wafanyabiashara kujitokeza na kujifunza mbinu mpya kutokana na ushauri wa kitaalamu wanaoupata pamoja na kubadilishana uzoefu na wenzao wenye mafanikio makubwa kuwazidi.

Shindano la Top100 huhusisha kampuni zenye mauzo ya kuanzia Sh1 bilioni hadi Sh20 bilioni na huratibiwa na kampuni ya kimataifa ya ukaguzi wa hesabu za fedha ya KPMG ikishirikiana na Mwananchi Communications Limited (MCL), wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti.

Miongoni mwa vigezo muhimu vinavyozingatiwa ni kuwa na hesabu za fedha zilizokaguliwa vizuri za miaka mitatu iliyopita na mfumo mzuri wa uongozi katika kampuni pamoja na mkakati wa kukuza biashara.

“Kwa vigezo vilivyopo, kampuni za kati zina uwezo wa kukua zaidi na kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa kutokana na uwezo wake wa kuajiri watu wengi,” anasema.

Mwaka huu shindano hilo linadhaminiwa na Benki ya NMB ambaye ndiye mzamini mkuu. Wadhamini wengine ni Hoteli ya Hyatt Regency, Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) na Azam TV.

Chanzo: mwananchi.co.tz