Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kampuni za bima nchini zahakikishiwa wateja

27273 Bima+pic TanzaniaWeb

Thu, 15 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mabadiliko ya Sheria ya bima katika uagizaji wa mizigo kutoka nje ya nchi huenda yakaleta ahueni kwa kampuni za bima nchini kwa kuwaongezea ukwasi kutokana na kuhakikishiwa upatikanaji wa wateja.

Mabadiliko hayo ya Sheria ya bima namba 10 ya mwaka 2009 kifungu cha 133 yaliyofanywa mwaka jana yanazitaka kampuni zote zinazoagiza mizigo kukata bima kupitia kampuni za bima za ndani tofauti na awali.

Akizungumza wakati wa mafunzo kwa wadau wa usafirishaji nchini, Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (Tira) Baghayo Saqware amesema mabadiliko hayo yamelenga kuongeza tija katika ukusanyaji wa mapato pamoja na kukuza biashara ya bima nchini.

Ametaja baadhi ya bidhaa yakiwamo magari na shehena ambazo kwa kawaida hulipiwa gharama ya ununuzi, bima pamoja na usafiri fedha ambazo ziliwanufaisha wauzaji wa nje.

"Kwa sasa mizigo yote itakatiwa bima kupitia kampuni za ndani, fedha iliyokuwa inapotea kutokana na kutumia bima za nje ni kubwa mno ni sawa na misaada ambayo tumekuwa tunaomba nje ya nchi," amesema Saqware.

Wakati mabadiliko hayo yakiendelea, utafiti wa mwaka 2012 wa Taasisi ya Usafiri Majini (Iscos) unakadiria zaidi ya Sh20 trilioni hupotea kutokana na matumizi ya bima za nje kwa kipindi cha miaka mitano.

"Kutumia bima za nje ni sawa na kuhamisha mitaji, lakini kwa kutumia kampuni za bima za ndani tunaongeza biashara ambayo itawawezesha kulipa kodi serikalini," amesema Saqware.

Rais wa Taasisi ya Bima Tanzania (IIT) Bosco Bugali amesema matumizi ya bima kutoka kampuni za ndani si tu yatakuza biashara bali ni msaada mkubwa kwa wafanyabiashara kuwa na uhakika wa mizigo yao hata kama vyombo vya usafiri vitapata hitilafu.

"Kuna majanga mengi yanaweza yakatokea, mfano; meli uliyoagizia mzigo imezama utakuwa umepata hasara na ndiyo maana tukaona kiwepo chombo kitakachotoa fidia kwa haraka," amesema.



Chanzo: mwananchi.co.tz