Serikali imemuagiza Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu kuyafanyia tathmini mashirika ya umma yaliyoshindwa kujiendesha, na kuisababishia Serikali hasara.
Agizo hilo, limetolewa hii leo Juni 17, 2023 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye utoaji wa gawio la Serikali na sherehe za miaka 25 ya Benki ya NMB.
Amesema, “Serikali imeunda mashirika haya ili yasaidie kupata fedha zitakazosaidia kubeba mzigo wa serikali na si mashirika kula serikalini bila kurudisha faida kwa hiyo msajili nimekupa baraka zote.”
Aidha, Rais Samia pia amesema Benki ya NMB ndio kiongozi nchini katika kutengeneza faida, na kwamba imeiweka nchi katika ramani ya kimataifa kwa kuwa ni benki ya tatu kwa faida katika sekta ya kibenki ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.