Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kampuni yaomba kuzalisha saruji Arusha

033470fbbb043af272de88fad2064ae8 Kampuni yaomba kuzalisha saruji Arusha

Thu, 12 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KUTOKANA na mahitaji makubwa ya saruji katika soko nchini, Kampuni ya Saruji Tanga, imeiomba serikali kufanikisha mazungumzo yao ya awali juu ya uwekezaji wa ujenzi wa kiwanda cha uzalishaji saruji jijini Arusha.

Mtendaji Mkazi wa kiwanda hicho, Ben Lema alisema Dar es Salaam kuwa, kampuni yake ina mpango wa kuongeza uzalishaji, lakini inasubiri mazungumzo ya awali baina yake na serikali juu ya uwekezaji kukamilika.

Alisema mradi wa ujenzi wa kiwanda hicho ukifanyika, utawezesha kuzalisha tani 500,000 hadi 750,000 kwa mwaka na kwamba, kiwanda hicho kitatoa ajira zaidi kwa Watanzania na kuchangia pato la taifa.

“Bado tuko kwenye mazungumzo na serikali juu ya mradi wa ujenzi wa kiwanda kipya cha saruji jijini Arusha kitakachosogeza huduma karibu zaidi kwa wananchi wa Kanda ya Kaskazini na maeneo mengine ya jirani mazungumzo hayo yameanza mwaka 2016 hadi sasa hatujayakamilisha. Tunataka kuendelea kumuunga mkono Rais John Magufuli juu ya azma ya Tanzania ya viwanda," alisema.

Kwa sasa Kiwanda cha Saruji Tanga kinasafirisha saruji yake katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini kwa kutumia treni ya mizigo iliyozinduliwa jijini Arusha hivi karibuni baada ya kutotumika kwa takribani miaka 30.

Kuhusu bei ya saruji kupanda nchini, Lema alisema kiwanda chao hakijapandisha bei. "Kwa sasa hatujapandisha bei za saruji, lakini tuna mpango wa kufanya hivyo Januari mwaka 2021 ili kusaidia wanahisa kupata gawio lao," alisema.

"Sababu mojawapo ya kupanda bei ya saruji ni wauzaji wa rejareja ambao wamekuwa wakinunua saruji kwa wingi kutoka kwa wasambazaji na kulangua," alisema.

Kipindi cha virusi vya corona, Kiwanda cha Saruji Tanga kilipata mahitaji makubwa ya saruji kiasi cha uzalishaji kufikia tani 108,000 kwa mwezi Oktoba kutoka tani 95,000 hadi 98,000 kwa mwezi.

Kiwanda hicho cha Tanga kinazalisha tani 1,250,000 hadi 1,260,000 za saruji kwa mwaka.

Chanzo: habarileo.co.tz