Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kampuni ya kizalendo kuwekeza kwenye katani

86858023da9332906e58422ec45ac2c2 Kampuni ya kizalendo kuwekeza kwenye katani

Fri, 18 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

Kampuni ya kizalendo ya KIKZ Promotion, imejitokeza kuwekeza katika ubunifu wa kuongeza thamani ya zao la mkonge.

Nayo Kampuni ya Mkonge kutoka Uholanzi, iitwayo Grosso Sisal Company imesema inatarajia kuwekeza Sh bilioni 132 kwenye ukuzaji wa zao hilo kwa kuanzisha viwanda vya kuchakata mkonge kwa lengo la kuliongezea thamani.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge nchini(TSB), Saddy Kambona alisema kampuni hiyo ya KIKZ ni ya Watanzania wasomi, ambao wamejikita katika ubunifu wa mitambo ya kuchakata zao la mkonge kwa kuongeza thamani ya zao hilo. Kwa kuanzia wametengeneza mashine za kutengeneza sukari inayotokana na mkonge pamoja na pombe.

"Haya ni maendeleo katika sekta ya kilimo cha mkonge kwa Watanzania kuja na ubunifu huo,"alisema.

Kambona alisema ugawaji wa maeneo katika mashamba matano ya mkonge wilayani Korogwe, umeanza mwezi huu na utakamilika Januari Mosi mwakani.

Alisema kuwa mchakato wa kuanza kugawa maeneo hayo ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alilolitoa Juni Mosi mwaka huu wakati akizindua Jengo la Bodi ya Mkonge (Mkonge House) na baada ya kutembelea Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI-Mlingano) wilayani Muheza, kinachojihusisha na utafiti wa afya ya udongo na mkonge.

Alisema kuwa maeneo yatakayotolewa ni katika mashamba manne ya Hale, Ngombezi, Magunga na Magoma.

Mashamba hayo yalikuwa yanamilikiwa na wakulima wadogo wa mkonge na Kampuni ya Mkonge ya Katani Ltd.

Alisema kuwa utaratibu wa fomu za maombi ya mashamba hayo, unapatikana katika tovuti ya Wizara ya Kilimo ambayo ni www.kilimo.go.tz ambapo wahitaji wanapakua fomu wanaijaza kisha wanaipeleka Bodi ya Mkonge wanapewa namba ya malipo.

Aliongeza: "Kwa watakaokosa maeneo hayo mchakato wa kugawa mashamba mengine ambayo hayajaendelezwa ambayo TSB watakabidhiwa na serikali utaendelea, hivyo wasiwe na wasiwasi,”

Chanzo: habarileo.co.tz