Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kampuni ya India yaingia soko la fedha la Tanzania

Kampuni India India.png Kampuni ya India yaingia soko la fedha la Tanzania

Tue, 12 Sep 2023 Chanzo: mwanachidigital

Wakati ambao huduma za kifedha kidijitali zinazidi kushika kasi, Kampuni ya Airpay Tanzania imetambuliwa na kupewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutoa huduma hiyo hapa nchini.

Airpay yenye makao makuu yake nchini India na kwa Tanzania ofisi Kuu zikiwa Zanzibar inaingia katika soka la huduma za fedha mtandaoni ambalo kwa sehemu kubwa hapa nchini linashikiliwa na huduma za simu na benki za kibiashara.

Akizungumza huko Zanzibar nchini Tanzania, Mwanzilishi wa Kampuni hiyo Kunal Jhunjhunwala anasema wanafuraha kupokea leseni hiyo ya huduma za malipo kutoka BoT na kwamba hiyo inaashiria kujitolea kwao katika kupanua huduma za kifedha kidijitali barani Afrika, huku Tanzania ikitumika kama lango lake kwa bara la Afrika.

“Binafsi nimejizatiti kufanya niwezavyo kuisaidia Tanzania kufikia malengo haya wakati kampuni yetu inapoanza safari yake kama mtoa huduma za malipo za Omnichannel hapa nchini, naamini sana katika ushirikiano na kuendeleza mfumo ikolojia unaowezesha kwa wote. " alisema Jhunjhunwala.

Kwa upande wake Mwanzilishi Mwenza wa Airpay Tanzania, Yasmin Chali alisema kampuni hiyo imejitolea kutoa suluhu za malipo za kiubunifu, salama na zinazoweza kufikiwa kwa biashara na watumiaji barani Afrika huku zikiunganisha huduma za kifedha ndani na nje ya bara hilo.

Anasema leseni hiyo ya huduma za malipo iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania inasisitiza kujitolea kwa kampuni hiyo kufuata mahitaji ya udhibiti wakati wa kutoa huduma za malipo ya kisasa.

Naye Makamu Rais na Meneja Mikakati wa kampuni hiyo, Mihayo Wilmore alisema leseni hiyo mpya inaipa kampuni uwezo wa kufanya kazi ndani ya mfumo ikolojia wa fedha wa Tanzania, na hivyo kuimarisha uwepo wake barani Afrika.

Alisema Airpay inajenga Makao Makuu ya Afrika yenye hadhi ya kimataifa visiwani Zanzibar, sambamba na Mpango wa Silicon Zanzibar. Kutoka katika kisiwa hicho cha paradiso, Airpay inalenga kufikia kila kona ya Afrika kupitia ushirikiano wa thamani.

“Safari hii haikuanza Februari, imekuwa na mchakato wa subira na machungu kwa miaka 30 iliyopita. Hakika tulikatishwa tamaa na hata kutaka kutupa taulo na kutoka nje ya ulingo. Airpay inaleta msisimko na hari mpya katika mfumo wa ikolojia wa kidijitali nchini Tanzania.

“Tulikuwa tumedumaa kama tasnia na kukimbilia kulalamika. Tunaishukuru serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mtazamo wake wa dira na kuweka vipaumbele vya kidigitali. Ninatazamia sana kufanya kazi na washirika wapya na wa zamani. Milango yetu iko wazi kwa ushiriki na ushirikiano,” anasema Wilmore

Akiizungumzia Airpay Wilmore alisema kampuni hiyo ina ushirikiano na taasisi za kifedha zaidi ya 200, na washirika wa kifedha zaidi ya 1000. Kimataifa Airpay inamtazamo wa kutanua nyayo zake katika Afrika na Mashariki ya Kati.

Chanzo: mwanachidigital