SERIKALI imepata hasara ya Sh bilioni 7.8 kupitia kampuni ya TANOIL ambayo ni tanzu kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC). Tanoil ilipewa jukumu la kufanya biashara ya uagizaji na usambazaji wa nishati ya mafuta.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Japhet Hasunga alisema hayo bungeni wakati anawasilisha taarifa ya Kamati kuhusu ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zilizokaguliwa za Serikali Kuu na Mashirika ya Umma kwa mwaka ulioishia Juni 30, mwaka jana.
Hasunga alisema katika mwaka wa fedha 2021/22, Tanoil ilipata hasara ya Sh bilioni 7.84 ukilinganisha na hasara ya Sh milioni 166.26 kwa mwaka wa fedha 2020/21.
Alisema hasara hiyo ilisababishwa na menejimenti ya Tanoil kutofanya usuluhisho wa kila mwezi wa mafuta yaliyonunuliwa na kuuzwa kwa kipindi husika. “Ukaguzi wa Juni 30, 2022 CAG alibaini kutofanyika usuluhishi wa mafuta ya thamani ya Sh bilioni 1.8,” alisema Hasunga.
Alitaja sababu nyingine ni kuchelewa kunakili mapato yatokanayo na uuzaji wa mafuta, kwamba CAG alibaini uwepo wa shehena mbili za mafuta ya Sh bilioni 16.1 ambayo ilipokelewa Juni 2022 lakini haikuandikwa kwenye vitabu vya uhasibu vya Tanoil hadi mwaka wa fedha unakamilika