Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kampuni kubwa nazo zipewe nafasi kutambua mchango wao

22424 Pic+kampuni TanzaniaWeb

Tue, 16 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwenyekiti wa kampuni ya Infotech Investnment Group, Ali Mufuruki amesifu shindano la Top 100 kutokana na mchango wake katika kuzijenga kampuni za kati kwa kuboresha mfumo wa uongozi na usimamizi wa mapato lakini akashauri hata kubwa pia zipewe nafasi ya kushindanishwa.

Hata hivyo anasema kutokana na manufaa yake, shindano hilo linatakiwa kupanuliwa kwa kuzishirikisha kampuni za wanawake na vijana.

“Kabla ya kuanzishwa kwa Top 100 kampuni nyingi zilikuwa zinatambuliwa kwa tuzo mbalimbali zilikuwa ni za kigeni hivyo kampuni za ndani zilisahaulika hususani ndogo na za kati ambazo hutoa ajira kwa wazawa wengi,” anasema Mufuruki.

Shindano la Top 100 ambalo huzijumuisha kampuni zenye mapato kati ya Sh1 bilioni hadi Sh20 bilioni kwa mwaka Mafuruki anasema lilikuja wakati sahihi kusaidia ukuaji na kutambua mchango wa kampuni za kati katika uchumi wa nchi.

Tangu mwaka 2011, anasema kampuni zilizoshiriki zimeelewa umuhimu wa kutunza kumbukumbu za fedha kwa kuwa ndicho kigezo kikuu cha kushiriki tena ziwe za miaka miwili, zilizokaguliwa.

“Kampuni ambazo hazikuwa na utamaduni wa kuhifadhi taarifa zake za fedha, waandaaji wa mashindano hayo huzijengea uwezo na kuziondoa woga,” anasema Mufuruki.

Anasema hofu iliyopo kwenye kampuni nyingi za kati kuweka wazi hesabu zake ni kudaiwa kodi stahiki na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) huku zikisahau manufaa yaliyopo.

“Kwa ujumla, shindano la Top 100 limesaidia kuziibua kampuni zilizokuwa zinaogopa kuweka wazi taarifa zake kwa umma, hata hivyo zilikuwa hazikui tofauti na baada ya kuelimishwa,” anasema.

Tuzo inayotolewa kwa washindi huongeza chachu na hamasa ya kushiriki kwani washindi huaminika zaidi kwa wateja, wabia hata taasisi za fedha hivyo kuwa tayari kufanya nazo biashara.

Kuongeza uwazi na kulipa kodi ya Serikali ambayo ni muhimu katika uchumi wa nchi kusaidia ujenzi wa miundombinu tofauti kuna manufaa mengi kuliko hasara tofauti na wajasiriamali wengi wanavyowaza.

Mufuruki anasema tuzo hizo ni fursa inayowakutanisha wafanyabiashara kutoka sekta binafsi, Serikali na vyombo vya habari kwa lengo la kukuza biashara nchini.

Anasema mwaka 2016 alihudhuria tuzo hizo kwa mara nyingine lakini alishtuka kuona idadi ya kampuni zinazoshiriki ikiwa ndogo.

“Hapa nchini kampuni zilizosajiliwa na Mamlaka ya Usajili na Leseni (Brela) ni takriban 100,000 lakini utashangaa ni kampuni 1,000 tu ndizo hushiriki tuzo hizo,” anasema Mufuruki.

Kutoakana na ukweli huo, anasema kuna umuhimu wa waandaaji kuongeza juhudi na kuzishirikisha kampuni za kibunifu hasa zinazotumia utaalamu wa kidijitali, viwanda na sanaa.

Anasema sasa ni wakati wa kuzishirikisha hata kampuni kubwa ambazo wigo wake tayari ni mpana lakini zinahitaji kutambuliwa na kulindwa ili ziendelee kuwa imara.

Anasema wakati wa maandalizi ya Top100 hata kama kuna changamoto waandaaji hawatakiwi kufa moyo kwani ni jambo lenye manufaa. “Kuna changamoto nyingi kama washiriki kutokuwa wengi na kukosekana kwa wadhani,” anasema.

Chanzo: mwananchi.co.tz