Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kampuni hewa sasa kufutwa

BRELA TZ Kampuni hewa sasa kufutwa

Tue, 7 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

SERIKALI imeagiza kufutiwa usajili kampuni zote zilizosajiliwa kwa ujanja ujanja ambazo zimekuwa hazihusishi tarifa na wala hazijulikani zilipo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Riziki Shemdoe, alisema hayo jana wakati akizungumza na viongozi na wafanyakazi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), jijini Dar es Salaam.

Shemdoe alisema kampuni hizo zimesajiliwa kwa ujanja ujanja na kutelekezwa na wahusika, hivyo kuna umuhimu wa kuandaa utaratibu wa kuhakikisha zote zinafutiwa usajili.

“Kama kuna ugumu wa kuzifuta kutokana na kanuni au sheria tuandikieni wizara ili Bunge lijalo tuwasilishe muswada tufanye marekebisho ya sheria tuzifute tubaki na kampuni halali zinazofanya kazi,” alisema Shemdoe.

Alisema anajua kwamba BRELA inadai fedha nyingi kwa kampuni hizo, lakini ikijaribu kuzitafuta hazizipati kwa sababu haziko popote.

Prof. Shemdoe pia aliwataka wafanyakazi wa BRELA kufanyakazi kwa uadilifu kwa kuwa taasisi hiyo inavishawishi vya rushwa, huku akisisitiza kuwa mtumishi yeyote atakayehusika na rushwa afukuzwe.

“Kama kuna mtu hawajibiki sehemu yake ashughulikiwe maana tumeingia kwenye uchumi wakati sasa tunapaswa kudhihirisha hili kwa kuhakikisha kila mtu anawajibika sehemu yake,” alisema.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa, alisema wamekuwa na mfumo wa usajili kwa njia ya mtandao (ORS) ambao unalalamikiwa sana na wateja kutokana na kutokuwa rafiki kwenye matumizi yake.

Alisema wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa taasisi hiyo wanausuka upya mfumo huo ili kuondoa kero zilizokuwa zinajitokeza mara kwa mara.

Nyaisa alisema kumekuwa na nyaraka ambazo zinahitaji kuandaliwa upya kwa kuwa zilizopo muda wake unakaribia kwisha na kumekuwa na nyaraka muhimu za kiutendaji ambazo hazikuwapo kabisa.

“Hali hii ilisababisha hata watoa maamuzi kufanya baadhi ya maamuzi kwa utashi wao bila kufuata sheria, kanuni na taratibu za kiutendaji,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live