Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kampuni 43 kuwania Tuzo za Chaguo la Mteja 2020

C74b765f3ca797f45f81ba7b9474161f.png Kampuni 43 kuwania Tuzo za Chaguo la Mteja 2020

Wed, 9 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KAMPUNI ya Lavine International Agency kwa ushirikiano na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) na wadau wengine imeandaa tamasha kubwa la hadhi ya kimataifa la utoaji wa Tuzo za Chaguo la Mteja mwaka 2020 litakalofanyika katika ukumbi wa Mtana katika jengo la Millennium Tower Dar es Salaam.

Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) ni wazalishaji na wasambazaji wa magazeti mahiri ya Daily News, HabariLEO, HabariLEO Afrika Mashariki na gazeti la michezo la kila wiki la SpotiLEO.

Tukio hilo kubwa na la kihistoria litakalofanyika Desemba 13, mwaka huu siku ya Jumapili litahusisha kampuni 43 ambazo zitakazobidhiwa tuzo zao kutokana na huduma bora walizotoa kwa wateja wao katika kipindi chote cha mwaka 2020.

Mkurugenzi Mtendaji wa Lavine International, Dayana Laiser alisema tuzo za chaguo la mteja au mlaji ni tuzo zitakazotolewa katika maeneo matatu ambayo ni kampuni bora, biashara bora na mfanyabiashara bora ambao jumla ni 43 kutoka katika kundi kubwa la washindani zaidi ya 270 waliojitokeza kuwania tuzo hizo.

Alisema kigezo kilichotumika katika kuwapata washindi ni kuangalia na kulinganisha huduma bora zinazotolewa na makundi yote matatu ambapo wateja waliopata huduma katika sehemu hizo walipiga kura kutaja mfanyabiashara yupi au kampuni ipi au biashara gani ilikuwa na huduma bora kwa wateja wake.

“Katika tuzo hizi tutakuwa na kampuni kubwa, kampuni za kati na kampuni ndogo zinazoibuka, tuzo hizi zitamulika kazi na vipaji ikiwa ni pamoja na kuongeza motisha na ubora katika utendaji,” alisema Laiser.

Alisema hiyo ni mara ya pili kwa kampuni hiyo kuandaa tamasha hilo na tofauti na mwaka uliopita, mwaka huu kutakuwa na ongezeko la washirika zaidi katika kuandaa na kufanikisha tamasha hilo. Miongoni mwa washirika hao ni pamoja na Absa Bank, Revolution Event, Plus Television na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN).

Meneja wa Mauzo na Masoko wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali, Januarius Maganga alisema TSN inajivunia kuwa mdau wa tuzo za mlaji ambapo imepata fursa ya ushirikiano na wadau muhimu kama vile benki ya Absa na wengineo.

Maganga alisema kwa hakika tuzo hizo zimeandaliwa kwa ubora wa hali ya juu na zinathibitisha kile kinachofanywa na kampuni na wafanyabiashara kwa wateja wao kwa kuwa sauti zao ndizo zilizofanikisha kupata washindi katika kinyang’anyiro hicho.

Alisema TSN kupitia magazeti yake ya Daily News na HabariLEO yamefanya jukumu kubwa katika kulitangaza tukio hilo ambapo mwitikio umekuwa mkubwa. “Nafarijika kuona mwitikio wa wananchi umekuwa mzuri na tumefarijika pia kuona kampuni 43 zitapata tuzo,” alisema Maganga.

Aliongeza kuwa mbali na majukumu hayo katika tukio hilo, TSN kupitia magazeti hayo imeendelea kufanya kazi yake vizuri na kwa umahiri mkubwa ya kuhabarisha, kazi ya kuelimisha na kazi ya kuburudisha.

Upigaji kura ulifanyika katika kipindi cha mwezi mmoja ambapo shughuli ilianza tangu Novemba 5 na kufungwa rasmi Desemba 6, mwaka huu.

Chanzo: habarileo.co.tz