Washiriki 420 kati ya 850 walioalikwa wamethibitisha kushiriki maonyesho ya Biashara ya Afrika Mashariki (MEATF) yatakayofanyika jijini Mwanza kwa wiki moja kuanzia Agosti 25, 2023 hadi Sepetemba 3, 2023.
Maonyesho hayo ya 18 yatakayofanyika katika uwanja wa Furahisha yatazinduliwa Agosti 29, 223 na Waziri wa Biashara, Dk Ashatu Kijaji.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza leo Julai 26, 2023, Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara wa Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Mwanza, Gabriel Mugini amesema washiriki 420 waliothibitisha kushiriki maonyesho hayo ni kampuni na wajasiriamali wadogo kutoka ndani na nje ya nchi.
Pamoja na wenyeji Tanzania, washiriki wengine ni kutoka nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan kusini na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
‘’Tumeboresha maonyesho ya mwaka huu kwa kufanyia kazi baadhi ya changamoto za maonyesho yaliyopita ikiwemo kuyahamishia uwanja wa Furahisha penye eneo na nafasi kubwa zaidi na kuondoa kiingilio kwa wananchi wanaotembelea maonyesho,’’ amesema Mugini
Amesema kupitia maonyesho hayo, wajasiriamali na wafanyabiashara nchini watapata fursa ya kujifunza na kuboresha eneo la vifungashio, utafutaji wa masoko na kuingia mikataba ya kibiashara na wenzao kutoka nje ya nchi wakati wa maonyesho hayo ya Kimataifa yaliyoanza mwaka 2006.
Akizungumzia maboresho kwa washiriki kutoka nje, Katibu wa TCCIA Mkoa wa Mwanza, Hassan Karambi amesema Serikali imeondoa vikwazo vyote vya mpakani kurahisisha uingiaji wa bidhaa za maonyesho kutoka nje ya nchi.
‘’Serikali imeondoa vikwazo vya mpakani kwa washiriki kutoka nje ya nchi; na TCCIA kwa kushirikiana na taasisi na mamlaka za Serikali tuko tayari kutoa msaada kutatua changamoto yoyote ya mpakani kwa washiriki kutoka nje ya nchi,’’ amesema Karambi
Mtendaji huyo wa TCCIA Mwanza amewaomba wafanyabiashara wadogo, kati na wakubwa kuendelea kujisajili katika Ofisi za taasisi hiyo ili kupata fursa ya kuonyesha bidhaa na huduma zao.
"Maonyesho ni fursa kwa wafanyabiashara wa ngazi zote kuonyesha na kuuza huduma na bidhaa zao. Pia kuna fursa ya kuingia mikataba ya Kitaifa na Kimataifa ya kibiashara na uwezekezaji na hivyo kutanua wigo na kuongeza tija,’’ amesema Hassan
Edda Raju, mkazi wa mtaa wa Nyakato jijini Mwanza ameupongeza uongozi wa TCCIA Mkoa wa Mwanza kwa kubuni maonyesho hayo akisema yanatoa fursa kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wa Tanzania kujifunza kutoka kwa wenzao kutoka nje ya nchi.
"Wananchi pia tunapata fursa ya kutembelea, kujifunza na hata kufanya manunuzi ya bidhaa kutoka ndani na nje ya nchi kwa bei nafuu tofauti na ile ya madukani,’’amesema Edda