Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kampuni 36 za India zashiriki maonyesho Dar

Mon, 25 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kampuni 36 kutoka India leo Ijumaa Februari 22, 2019 zimeshiriki maonyesho ya kimataifa ya biashara yanayofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.

Maonyesho hayo ambayo yanafanyika kwa siku mbili, yamehusisha kampuni nyingine kutoka nchi ya Afrika Kusini, Saudi Arabia, China, Poland na nchi mwenyeji Tanzania.

Bidhaa zaidi ya 300 zimeonyeshwa na washiriki mbalimbali katika maonyesho hayo ambayo yamehusisha sekta kubwa kama kilimo, ujenzi na viwanda.

Akizungumza na Mwananchi katika maonyesho hayo, mkurugenzi msaidizi wa kampuni ya FIEO kutoka India ambayo ndio imeratibu safari ya wafanyabiashara kutoka India kuja Tanzania, Sunita Tatwal, amesema, "Kuna mabadiliko makubwa kwenye idadi ya washiriki kutoka India mwaka huu pamoja na idadi ya bidhaa zilizoonyeshwa.” Amesema mwaka jana kampuni 34 zilishiriki.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa Taasisi ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoa wa Dar es Salaam, Francis Lukwaro amewataka wafanyabiashara kutoka Tanzania kutumia fursa ya maonyesho hayo katika kutafuta fursa mpya za biashara.

Pia ameeleza Januari, 2019, TCCIA ilisaini mkataba na taasisi ya biashara kutoka India,  kwa lengo la kuwaunganisha wafanyabiashara kutoka India na Tanzania kufanya uwekezaji wa pamoja.

Mmoja wa wafanyabiashara kutoka India, Asit Kumar amesema anatarajia kutengeneza mahusiano mazuri na wadau wa biashara kutoka Tanzania ikiwa lengo ni kubadilishana ujuzi na bidhaa.

Pia mshiriki mwingine kutoka India Nikhil Punamiya amesema, "Tanzania kuna soko zuri la kufanya biashara. Tutaanza kuleta bidhaa kuuza hapa. Tukipata fedha za kutosha, tutatengeneza kiwanda cha nguo hapa. " amesema.

Kwa upande mwingine, balozi wa India nchini Sandeep Arya akiambatana na Raisi wa TCCIA, Octavian Mshiu walitembelea maonyesho hayo na pia walipata fursa kutembelea kwenye baadhi ya vibanda vya wafanyabiashara kutoka India.



Chanzo: mwananchi.co.tz