Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kampuni 29 za Uturuki zatafuta fursa Tanzania

Kampuni Madiniiii Kampuni 29 za Uturuki zatafuta fursa Tanzania

Thu, 6 Jun 2024 Chanzo: Mwananchi

Kampuni 29 kutoka nchini Uturuki zimekuja Tanzania kwa ajili ya kutafuta fursa za uwekezaji na ubia kutoka kwa wafanyabiashara nchini katika sekta za viwanda, kilimo na afya.

Wawakilishi kwa kampuni hizo ambazo zimefanya mazungumzo na wafanyabiashara mbalimbali jijini hapa wamekuja ikiwa ni siku chache tangu Rais Samia Suluhu Hassan kufanya ziara ya kikazi katika nchi hiyo kati ya Aprili 17 hadi 21 mwaka huu.

Samia alitembelea nchi hiyo kwa mwaliko wa Rais mwenyeji Recep Tayyip Erdoğan ambapo miongoni mwa aliyoyafanya ni kuwaita wawekezaji kuja kuchangamkia fursa zinazopatikana Tanzania.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana Juni 5, 2024 inaeleza kuwa, mbali na kuzungumza na wafanyabiashara wa ndani, kampuni hizo zimeonyesha nia ya kushiriki maonyesho ya kimataifa ya biashara maarufu Sabasaba ili kuweza kutafuta wateja zaidi wa bidhaa wanazozalisha.

Akilizungumzia hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Viwanda na Biashara (Tantrade), Latifa Khamis amesema kampuni hizo zimeona fursa iliyopo Tanzania na zipo tayari kuzitumia.

“Wenzetu wanapokuja kufanya biashara wanahakikisha kwamba hata kama hawajauza ila wamepata mbia au anaondoka na mtu ambaye atakua mdau au mnunuzi wa bidhaa zao ambaye badala ya yeye kusafiri kufuata mzigo, ataagiza na ataletewa, huu ujio ni mzuri kwetu kiuchumi,” alisema Latifa.

Wakati Latifa akiyasema hayo tayari Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuongeza kiwango cha ufanyaji biashara hadi kufikia Sh2.5 trilioni kwa siku za usoni kutoka Sh890.1 bilioni mwaka uliopita.

Makubaliano hayo yalifikiwa nchini Uturuki baada ya Rais Samia na mwenyeji wake Erdoğan kufanya mazungumzo ya pamoja kabla ya kutoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari.

Makamu Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Abdul Mwilima alisema kwa sasa biashara kati ya nchi hizo mbili imeendelea kuimarika kutokana na Watanzania kuanza kununua bidhaa za nguo na mashine kutoka Uturuki.

“Watu wengi walikuwa wanaenda China kutafuta nguo lakini wametambua kuwa Uturuki inatengeneza nguo, viatu na bei zao ni nzuri sambamba na mashine,” alisema Mwilima.

Kwa upande wake Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Mehmet Gulluoglu alisema wameamua kuja kutafuta fursa nchini Tanzania kwa sababu ni kitovu kwa nchi ambazo hazina bahari.

Chanzo: Mwananchi