Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kampuni 18 za Tehama kushiriki maonyesho ya ubunifu

Tue, 13 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Zaidi ya Kampuni 18 za Tehama zitashiriki maonyesho ya mawasiliano wiki hii yatakayotoa fursa kwa wabunifu kuendeleza kazi zao.

Maonesho hayo yatahusisha kampuni za simu, watoa huduma za mitandao pamoja na taasisi ikiwamo Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) yatafanyika kwa siku mbili kuanzia Novemba 15 hadi 17, 2018.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne, Novemba 13, Meneja Mradi wa Kampuni ya Aecco Consulting Ltd ambao ni waandaaji wa maonesho hayo, Jacqueline Buretta amesema ni fursa kwa wabunifu kuendeleza kazi zao.

"Tumeona tutoe fursa kwa wananchi kununua bidhaa na kukutana na wadau mbalimbali ambao watasaidia kupata majibu ya changamoto mbalimbali za kiteknolojia" amesema.

Maonesho hayo yatatoa fursa kwa wanafunzi wa Tehama kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Ndaki ya Tehama (Coict) kuonyesha ubunifu wao huku wakiwa na uhakika wa kupata chapuo kutoka kwa wadau wakubwa.

Naye Ofisa Masoko wa Kampuni ya Jumia, Kijanga Geofrey amesema maonesho hayo yatasaidia kuleta mapinduzi ya biashara kupitia teknolojia ya mtandao.

"Teknolojia inakua kwa kasi na imepunguza muda kwa watu kutafuta bidhaa ambazo kwa sasa zinaweza kumfikia mahali popote kwa kutumia simu," amesema.

Baadhi ya kampuni zitakazoshiriki ni Tigo, Jumia, Kituo cha Taifa cha Data, Smile Communication, Benki ya Equity, Kampuni ya TTCL pamoja na taasisi mbalimbali.



Chanzo: mwananchi.co.tz