Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kampuni 16 za Austria zatua Tanzania kusaka fursa

Thu, 31 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kampuni 16 kutoka Austria zimekuja nchini kusaka fursa za uwekezaji katika maeneo tofauti, zaidi katika sekta ya viwanda kutokana na kuzalisha kwa wingi mashine.

Kampuni hizo leo Jumatatu Januari 28, 2019 zilikutana na chemba ya wafanyabiashara wakulima na wenye viwanda (TCCIA) katika kongamano lililoandaliwa na wizara ya mambo ya nje.

Katika mkutano huo, mkurugenzi wa uhamasishaji wa uwekezaji wa kituo cha uwekezaji (TIC) John Mnali amesema Austria kama nchi ambayo imeendelea katika masuala ya teknolojia, Tanzania inaweza kunufaika na maendeleo hayo kupitia uwekezaji.

“Ni taifa ambalo kampuni zake zinafanya vizuri kwenye  viwanda, ufuaji wa umeme wa maji, usambazaji wa bidhaa na uzalishaji wa mashine zenye uwezo wa kuzalisha mashine tofauti,” amesema Mnali.

Hata hivyo katika mkutano huo ofisa wa uhamasishaji wa TIC Diana Mwamanga amesema miongoni mwa fursa za uwekezaji ambazo kampuni hizo zinaweza kunufaika nazo ni viwanda vya kuunganisha magari, bidhaa za tiba na dawa, uzalishaji wa sukari na mafuta ya kupikia.

Pia alizitaja fursa nyingine kuwa ni uvuvi, ufugaji na bidhaa za ngozi. Maeneo hayo yalitajwa kuwa na fursa nyingi kwa kuwa uwekezaji si mkubwa na hata uzalishaji bado hautoshelezi mahitaji.

Kaimu Rais wa TCCIA, Octavian Mshiu amesema tayari kuna kampuni ya Austria inayobangua korosho hapa nchini lakini kutokana na ujio wa kampuni hizo uwekezaji utaongezeka zaidi hususani katika sekta ya kilimo na viwanda.

“Austria ina watu takribani milioni 8.4 hivyo si fursa kubwa kwetu kuuza bidhaa huko lakini kwa kuwa wameendelea katika teknolojia tukishirikiana nao ni fursa kwetu katika uwekezaji hapa nchini,” amesema Mshiu.

Mkurugenzi wa chemba ya uchumi wa Austria wa kanda ya Afrika na Mashariki ya Kati, Nella Hengstler amesema shughuli kuu ya uchumi katika nchi yao ni utengenezaji wa mashine na bidhaa za plastiki.

“Kwetu kilimo ni sekta ndogo, uchumi wetu unategemee sana utengenezaji wa mashine na uuzaji bidhaa nje ya nchi ikiwemo vipuli vya magari. Afrika huuza zaidi maua na bidhaa za kilimo nchini kwetu,” amesema Hengstler.



Chanzo: mwananchi.co.tz