Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kampuni 15 zajitosa kubangua korosho

Fri, 21 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mtwara. Kampuni 15 zimejitokeza kuomba kubangua korosho zilizonunuliwa na Serikali huku baadhi ya wabanguaji wadogo wakiwa tayari wameshabangua magunia sita ya majaribio.

Hayo yameelezwa leo Ijumaa Desemba 21, 2018 na Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya wakati akipokea korosho tani tisa katika ghala la Shirika la kuhudumia viwanda vidogo vidogo (Sido) Mtwara ambapo kazi rasmi ya ubanguaji itaanza leo.

Manyanya amesema katika kampuni hizo wako katika kuweka mikataba ikae vizuri na wale watakaotembelewa na kujiridhisha ndipo watapewa mikataba.

“Katika shughuli ya ubanguaji tunategemea kutumia makundi mawili, kundi la wenye viwanda na akina mama ambao wamekuwa wakifanya shughuli za ubanguaji kila siku.”

“Sasa hivi tumeshajipanga kuanza shughuli ya ubanguaji kuwa endelevu katika eneo hili la Sido na mzigo tumeshachukua,” amesema Manyanya.

Amesema korosho zitabanguliwa katika maeneo mbalimbali nchini baada ya kutembelea vikundi na kujiridhisha kuwa kikundi kinaweza kufuata masharti yote ya ubanguaji na kuweka chakula katika mazingira sahihi.

“Kwa sababu huu ni mwaka wa kwanza yawezekana hatutabangua korosho yote lakini sehemu kubwa tutakuwa tumejifunza na tumeshaweka msingi wa Tanzania kurudi katika kubangua korosho yetu na kuiongezea thamani lakini pia kutoa ajira,” amesema Manyanya.

Mkurugenzi Mkuu wa Sido, Silvester Mpanduji amesema jukumu lao ni kusimamia viwanda vidogo vifanye kazi.

Amesema kufungwa kwa viwanda vingi miaka ya nyumba kulitokana na wabanguaji wadogo kushindwa kupata korosho lakini sasa vitaanza kufanya kazi.

Amesema viwanda vya maeneo ya Sido vitatoa ajira 100 katika kazi nzima ya kubangua lakini watahakikisha wanatafuta viwanda vingine ambavyo watavisimamia kuhakikisha vinapata korosho ya kutosha.

“Korosho tuliyopokea tani tisa tunatarajia wataibangua kwa takribani wiki moja kufuatana na makubaliano ambayo tumefanya na baada ya wiki moja tena tutapokea tani tisa nyingine na hivi viwanda vidogo tunataka vijenge tabia ya kulipa kodi kama sehemu ya makubaliano,”amesema.

Mmoja wa wabanguaji katika eneo la Sido, Siwa Rajab amesema siku za nyuma walipewa msaada wa mashine 54 za kubangua korosho lakini zilikuwa hazifanyi kazi kutokana na wao kushindwa kumudu gharama za kununua korosho katika minada.

“Korosho kubaki Tanzania sisi tunapata ajira na mashine zetu zitafanya kazi na wa mama wengi watapata ajira, majumbani huko mambo yatakuwa mazuri,” amesema.

Amesema uwezo wa kikundi kununua korosho tani 50 hatuna kwa hiyo tulikuwa tunaishia kubangua korosho zetu za shambani zikiisha tunakaa hata kabla msimu kuisha.



Chanzo: mwananchi.co.tz