Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kamishna TRA awataka wazalishaji kutumia ETS

79501 TBL+PIC

Fri, 11 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dk Edwin Mhede amewataka wazalishaji wanaotakiwa kutumia stampu za kodi za kieletroniki (ETS), kuendelea kuzitumia kama sheria na taratibu za kodi zinavyoelekeza.

Amesema kwa jicho la ndani, stemp hizo zina faida kubwa kwa wazalishaji na zinawawezesha kufahamu bidhaa halisi zinazoingia sokoni ili kulinda viwanda vyao.

Dk Mhede aliyasema hayo jana Jumatano Oktoba 9, 2019 alipotembelea kiwanda cha kuzalisha bia (TBL) mkoani Mbeya, kujionea namna stempu za kodi za kieletroniki zinazofanyakazi katika kiwanda hicho.

Alisema ETS inasaidia kukusanya taarifa sahihi si kwa matumizi ya kukadiria kodi pekee, bali inamsaidia pia mzalishaji kujua kiasi alichozalisha, na kwa muda gani. Lakini pia itamsaidia kuona kama kuna changamoto yoyote aweze kuifanyia kazi mapema kitu ambacho ni muhimu katika shughuli za uzalishaji.

“ujumbe wangu kwa wazalishaji wengine ni kwamba, waendelee kutumia stampu za kodi za kielektroniki kama ilivyoelekezwa na sheria na taratibu za kodi kwa kuwa inasaidia kuongeza ufanisi katika uzalishaji na kuweka taarifa sahihi za uzalishaji”, alisema kamishna huyo.

Hata hivyo, alisema katika matumizi ya mifumo, changamoto hazikosekani lakini ni vema kutumia na kufahamu changamoto zilizopo na kuzifanyia kazi kwa kuwa si vibaya kuboresha mifumo pale patkapogundulika kuna changamoto katika matumizi ya mfumo huo.

Pia Soma

Advertisement
Naye Meneja wa kiwanda hicho, mkoani Mbeya, Godwin Fabian alisema TBL inaamini kuwa ETS ni msaada mkubwa kwa wazalishaji kwa kuwa inawezesha kugundua bidhaa zisizo halali na zinazoingia sokoni bila kufuata taratibu za uzalishaji na ulipaji kodi.

“Ujumbe wangu kwa wazalishaji wengine waone ni kitu kizuri na wasiogope kutumia stempu za kodi za kieletroniki kwa kuwa kama bidhaa zote zitawekwa stempu hizi, itasaidia kufahamu bidhaa zisizo halali zinazoingia sokoni na hivyo mfumo huu utasaidia kukabiliana nazo,” alisema Fabian.

Matumizi ya ETS kwa bidhaa zinazotozwa ushuru yalianzishwa kwa lengo la kuchukua nafasi ya matumizi stempu za karatasi ambazo matumizi yake yalihusishwa na vitendo vya ukwepaji kodi pamoja na bidhaa bandia kwa kiasi kikubwa.

Hii ni mojawapo ya hatua ya Serikali inayolenga kuboresha usimamizi wa kodi nchini. Wanufaika wa mfumo huu ni Serikali, wazalishaji, waagizaji na watumiaji na faida zake ni kulinda mapato ya Serikali kwa kuzuia bidhaa bandia, kumuwezesha mtumiaji kutambua bidhaa yenye stempu halali kwa kutumia simu ya mkononi pamoja na kuongeza uhiyari wa ulipaji kodi kwa kutengeneza wigo sawa wa ushindani kwa wafanyabiashara wanaozalisha na kuingiza bidhaa nchini.

Faida nyingine ni kuwezesha ufuatiliaji wa bidhaa kutoka viwandani, mipakani, bohari zilizoruhusiwa, majengo ya kutunzia bidhaa, sokoni hadi kwa mlaji na kuwezesha usimamizi wa bidhaa zinazotengenezwa au zinazoingizwa kutoka nje ya nchi.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz